Lissu akwama kuzuia ushahidi wa Jamhuri

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekwama katika harakati zake za kutaka kuzuia sehemu ya ushahidi wa Jamhuri, akidai kuwa hauhusiani na shtaka linalomkabili la uhaini.

Lissu ameibua pingamizi mara mbili dhidi ya shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi hiyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, George Bagemu wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo, inayosikilizwa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Hata hivyo mahakama hiyo imetupilia mbali hoja za Lissu huku ikikubaliana na hoja za Jamhuri zilizotolewa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, kuwa mamlaka ndio inawajibu wa kuamua kuhusu ushahidi huo kama una uhusiano na shtaka au la.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kesi  hiyo ya  inayosikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, imeanza  kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri leo.

Wakati akitoa ushahidi wake, shahidi hiyo wa kwanza wa Jamhuri, Bagemu ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum Dar es Salaam (DZCO), Lissu amesimama  na kuweka pingamizi kwa sehemu ya maelezo ya ushahidi wake.

Katika ushahidi huo shahidi amerejea maneno aliyomo kwenye kipande cha picha jongefu (video clip) inayomuonesha Lissu akizungumza maneno mbalimbali yakiwemo yaliyomo kwenye hati ya mashtaka.

Lissu ameweka pingamizi katika maelezo ya shahidi huyo kuwa alimsikia Lissu akisema kuwa mapolisi wanabeba vibegi mgongoni vikiwa na kura bandia na kuingia navyo kwenye vituo vya kura.

Lissu amepinga maneno hayo akidai kuwa yeye anashtakiwa kwa mashtaka ya uhaini na maneno hayo aliyoyasema shahidi si miongoni mwa maneno yaliyoko kwenye hati ya mashtaka.

Hivyo, amedai kwamba hayahusiani na shtaka na hayapaswi kuingizwa kwenye kumbukumbu za mahakama.

Akijibu hoja hiyo ya pingamizi hilo la Lissu, wakili Katuga amedai kuwa ni jukumu la Jamhuri kuthibitisha kesi yake na kwamba shahidi ataulizwa maswali na hatakiwi kupangiwa cha kusema.

Wakili Katuga amedai kuwa shahidi bado anaendelea kutoa ushahidi na ana haki ya kutoa ushahidi na hawezi kuchaguliwa sehemu ya ushahidi wa kutoa.

Akijibu hoja hiyo ya wakili Katuga, Lissu amesisitiza hoja yake kuwa maneno hayo kwa kuwa hayako kwenye hati ya mashtaka hayahusiani na shtaka na kwamba kwa mujibu wa sheria hayapaswi kuruhusiwa.

Lissu amesisitiza  kuwa maneno hayo yakiruhusiwa yanaweza kutoa mwanya kwa upande wa mashtaka kuingizwa ushahidi mwingine wa mambo yasiyoyalalamikiwa.

Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Ndunguru amesema ni jukumu la mahakama kuamua kama ushahidi huo hauhusiani na shtaka ama la.

Jaji Ndunguru amesema kuwa shahidi bado anaendelea na ushahidi na haijajulikana atafikia wapi, huku akisema kuwa bado mshtakiwa atapata nafasi ya kumuhoji maswali ya dodoso kuhusiana na hoja yake hiyo.

“Hivyo pingamizi hilo linakataliwa, kwani mahakama ndio itaamua kama ushahidi huo unahusiana au hauhusiani na shtaka”, amesema Jaji Ndunguru. Baada ya uamuzi huo shahidi huyo ameendelea kutoa ushahidi na akiongozwa na Wakili Katuga kwa maswali ya kumuongoza kutoa ushahidi wake huo.

Katika mwendelezo wa maelezo ya ushahidi wake shahidi huyo amedai kuwa, kauli nyingine aliyoisikia Lissu akitoa katika video hiyo ni kwamba majaji ni watu wa rais na wao ni maCCM na hupenda kuteuliwa kwenda Mahakama ya Rufaa.

Kwa mara nyingine tena Lissu amepinga maelezo hayo.

“Waheshimiwa majaji wajibu wangu mimi mi kupinga. Na hili napinga kuwa majaji ni watu wa raisi na wao ni maCCM halipo kwenye hati ya mashtaka, hivyo hayahusiani na shtaka. Naiomba mahakama isiruhusu kila takataka kuingizwa kwenye kumbukumbu za mahakama”, amesema Lissu. Hata hivyo mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo.

Jaji Ndunguru amerejea majibu na msimamo wa uamuzi katika pingamizi la awali akisisitiza kuwa mahakama ndio yenye nafasi ya kuchambua ushahidi na kujua kama unahusiana au hauhusiani na shtaka.

Hivyo shahidi huyo ameendelea na ushahidi wake huo akiongozwa na Wakili Katuga, ambapo ameelezea pamoja na mambo mengine hatua alizozichukua baada ya kuangalia video hiyo.

Katika kesi hiyo Lissu anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa lengo la kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchapisha  maneno yafuatayo:-

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Lissu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na kusomewa shtaka hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, alikofikishwa kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilisha upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, kwa ajili ya usikilizwaji kamili.

Baada ya upelelezi kukamilika kesi hiyo ilihamishiwa rasmi Mahakama Kuu Agosti 18, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji kamili.