Mapema tu Msauzi ashtua Simba, vigogo wakutana ghafla

DAKIKA 450 sawa na mechi tano zimetosha kumfanya beki mpya wa Simba, Rushine De Reuck kuwashtua vigogo wa timu hiyo na kuamua kuitana ghafla chemba.

Kuitana kwa mabosi hao ni baada ya kuridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na beki huyo wa kati kupitia mechi tano za mashindano zilizopita ambapo amefanikiwa kufunga mabao mawili.

Baada ya kuridhishwa na uwezo wake, mabosi wa klabu hiyo fasta wameamua kufanya jambo ili kujiweka salama kwa Msauzi huyo.

Rushine ni mmoja ya nyota wapya 13 waliosajiliwa dirisha la usajili lililofungwa Septemba 7 na tangu aanze kukiwasha amekuwa gumzo kwa kiwango alichokionyesha na kwa sasa anamiliki mabao mawili aliyofunga katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate na Namungo.

Kutokana na kiwango alichokionyesha beki huyo aliyesajiliwa kutoka Mamelodi Sundowns aliyotwaa nao jumla ya mataji nane, yakiwamo matano ya Ligi Kuu ya Sauzi, MTN8 Cup, Nedbank Cup na African Football League, kimewafanya mabosi wa Simba kumuita mezani haraka.

RUSH 01


Lengo la kumwita mezani beki huyo ni kutaka kuurefusha mkataba alionao, kwani awali inadaiwa walimchukulia poa na kumpa mkataba mfupi na hofu ni kuja kushikwa masikio na wajanja kisha kuwapa wakati mgumu kutaka kumbakisha kikosini.

Rushine kabla ya kuja Simba kutokea Mamelodi alikuwa akikipiga Maccabi Petah Tikva ya Israel alikokuwa akiitumikia kwa mkopo na alipendekezwa na Kocha Fadlu Davids aliyeondoka Msimbazi.
Inadaiwa Simba ilikuwa na wasiwasi na beki huyo kutokana na taarifa alikuwa na rekodi za kuwa majeruhi mara kwa mara, hivyo kumpa mwaka mmoja ili kumsikilizia, lakini kwa kiwango alichokionyesha wanaona ni vyema kukaa naye ili kumwongeza zaidi mapema.

RUSH 03


Simba inataka kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja au miwili, endapo watakubaliana naye kwa lengo la kutaka aendelee kupiga kazi Msimbazi kwa muda mrefu.

Inaelezwa sababu ya mabosi wa Simba kutaka kumuwahi mapema Rushine ni kuhofia huenda ofa zitakazotua kwake kutoka nje ya klabu hiyo zinaweza kuwasumbua mwishoni mwa msimu iwapo watampa mkataba mpya sasa.

RUSH 02


Taarifa kutoka Simba zimeiambia Mwanaspoti; “Ameanza vizuri mno, tulikuwa na wasiwasi kabla lakini wakati huu kila mmoja ameona kiwango chake Rushine na tumeridhika.

“Ameanza katika mechi zote ndiyo maana tumeshamwambia sasa tunataka tumpe mkataba mrefu abaki hapa zaidi, hivyo muda wowote tunaweza kumalizana naye iwapo ataafiki kumwongezea.”

Rushine katika mechi tano za mashindano amecheza kwa muda wote akitumia dakika 450, huku ukuta anaoulinda akishirikiana na Abdulrazak Hamza na Chamou Karaboue ukiruhusu mabao mawili likiwamo lile la Ngao ya Jamii la Pacome Zouzoua wa Yanga na jingine na Gaborone United katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba ikipata sare ya 1-1 nyumbani.