Mashindano maarufu ya Vodacom Tanzania Open 2025 yamehitimishwa katika mandhari ya kuvutia ya Kilimanjaro Golf & Wildlife Estate (Kiligolf) jijini Arusha kwa hafla ya utoaji wa zawadi iliyoambatana na shamrashamra. Mashindano haya ya siku nne yaliwaleta pamoja wachezaji wa golf wa rika na viwango tofauti kutoka maeneo mbalimbali ya Africa, yakifungua ukurasa muhimu katika kalenda ya golf hapa nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Vodacom Tanzania PLC, Bw. David Tarimo, aliyaelezea mashindano hayo kuwa ya mafanikio makubwa, “tumekuwa na siku nne za kipekee. Tumeshuhudia ushindani wa kusisimua, vipaji vya kustaajibsha na shauku kubwa kwa michezo. Kuanzia wachezaji wa kitaalamu hadi wale wanaochipukia, mashindano haya yamewaleta pamoja washiriki wa aina mbalimbali wapatao 150, na kuyafanya kuwa miongoni mwa mashindano ya kukumbukwa zaidi.”
Aliendelea kusisitiza dhamira ya Vodacom katika michezo na teknolojia akisema, “golf inaakisi maadili yetu tunayoyathamini, usahihi, nidhamu na fikra za kimkakati. Kama mdhamini kwa mwaka wa tatu mfululizo, tunawekeza katika jukwaa linaloinua vipaji vya ndani, linakuza ushirikiano wa kikanda, na kuiweka Tanzania kama kituo cha matukio ya michezo ya kiwango cha kimataifa. Mwaka huu, tumeunganisha teknolojia ya kisasa katika mashindano haya kuanzia taarifa za matokeo ya moja kwa moja hadi uzoefu wa mashabiki unaoendeshwa na mtandao wa Vodacom.”
Mashindano ya Vodacom Tanzania Open 2025 yamesajiliwa katika viwango vya World Amateur Golf Ranking (WAGR) na yanaendana na dhamira pana ya Vodacom ya kuwawezesha jamii kupitia michezo, ujumuishaji na matokeo chanya endelevu.
Akiongeza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Golf nchini Tanzania (TGU), Bw. Gilman Kasiga, alisifia ushirikiano huo na mchango wa mashindano hayo katika mchezo wa huo nchini, “tunajivunia kushirikiana na Vodacom Tanzania kwa mashindano ya mwaka huu. Dhamira yao ya ubora na ubunifu imepandisha kiwango cha mashindano ya golf nchini. Tukio hili limeonyesha vipaji vya hali ya juu na pia limeonyesha jinsi ushirikiano wa kimkakati unavyoweza kukuza michezo na kuhamasisha jamii. Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Vodacom imesimama nasi, ikionyesha kujitolea kwake katika kukuza michezo na vipaji hapa nchini.”
Mashindano haya yametoa zawadi kubwa kwa washindi wa makundi ya kitaalamu na ya ridhaa, ambapo washindi wa juu wa kitaalamu walipokea hadi shilingi 8.2 milioni, huku zawadi za fedha zikitolewa kwa washiriki 22 wa juu. Mshindi wa juu wa ridhaa pia alitunukiwa zawadi ya shilingi 2.5 milioni, ikionyesha dhamira ya mashindano haya ya kusherehekea ubora katika viwango vyote vya mchezo.
Washindi walipatikana kwa kuzingatia matokeo ya siku nne za mchezo wa stroke play, kwa mujibu wa kanuni za Golf zilizopitishwa na R&A na USGA, na zikisaidiwa na kanuni za ndani za Kiligolf.
Kadri Vodacom inavyosherehekea miaka 25 ya kuwaunganisha Watanzania, kampuni hiyo inaendelea kujenga urithi wa ubora katika uwanja wa golf, ndani ya jamii na katika ukanda mzima wa Afrika mashariki.
Washindi wa Vodacom Tanzania Open 2025 wakiwa katika picha ya pamoja jijini Arusha, wakiwemo Njoroge Kibugu (Kenya) kwa upande wa wanaume na Madina Idd (Tanzania) kwa upande wa wanawake. Mashindano haya yalishirikisha wachezaji zaidi ya 150 kutoka nchi nane barani Afrika, yakionyesha vipaji vya kipekee na ushindani wa hali ya juu