Mwalimu aahidi Serikali yake kukomesha ugumu wa Maisha

Dar es Salaam. Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameahidi kupambana na ugumu wa maisha unaolikumba Taifa, hususan mfumuko wa bei ya chakula katika Jiji la Dar es Salaam, endapo atachaguliwa kuwa Rais.

Amesema Wananchi wa Jiji hilo, wanakumbwa na ugumu wa maisha unaochangiwa na kuongezeka kwa bei ya vyakula muhimu, hali inayoathiri zaidi kipato. Mfumuko wa bei ya chakula umekuwa ukipanda kwa kasi na kusababisha changamoto kwa familia kupata mlo kamili kwa siku.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kimara Suka, Ubungo, Leo Oktoba 06, 2025 Dar es Salaam Mwalimu ameeleza kuwa serikali yake itakuwa ya wananchi, itakayotoa fursa ya kujitafutia kipato halali bila kubughudhiwa.

“Mungu akijalia nikiwa Rais, chochote kinachomwingizia mtu kipato alimradi si bangi wala madawa ya kulevya, mtu aachwe ajitafutie riziki. Mtu anabanwa nitawaacha,” amesema Mwalimu.

Mwalimu ameelezea changamoto kuu atakazopambana nazo akiwa Rais, ikiwa ni pamoja na Mfumuko wa bei ya chakula, Kodi kubwa na gharama za makazi, Miundombinu mibovu ya barabara, gharama ya usafiri na gharama za maisha kwa ujumla.

Amesema serikali ya sasa imeshindwa kusimamia rasilimali za wananchi, badala yake imewekeza nguvu zote Dar es Salaam huku ikiwasahau wananchi wa mikoani

“Gharama ya maisha Dar es Salaam imepanda; Sh5,000 haiwezi kukuwezesha kurudi nyumbani na kitu cha maana. Hii ni pamoja na kodi ya nyumba, ushuru, na bei ya chakula. Hali hii ni mbaya sana,” amesema

Mwalimu ameahidi kuongeza uzalishaji wa chakula kwa wingi ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa bei nafuu, huku akiwataka Watanzania kuikataa CCM na kumpa nafasi ya kuleta mageuzi ya kweli

“Msela nitinge Ikulu, tuje tushughulikie mfumuko wa bei, hasa eneo la chakula… Wakati wa mabadiliko ni sasa.”

Rungwe: “Watanzania Amkeni!”

Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe, alitumia jukwaa hilo kuwaasa Watanzania kuachana na CCM, akiwaita kuwa ni “maharamia” wanaodanganya kwa ahadi zisizotekelezeka.

“Haiingii akilini kwa chama kilichotawala kwa miaka 64 kuahidi kuboresha soko la Kimara wakati kero hizo zimekuwepo kwa muda mrefu. Hiyo ni danganya toto,” amesema Rungwe.

Naye Edward Kinabo, mgombea ubunge wa Kibamba kupitia chama hicho, amekosoa vikali hali ya miundombinu, maji na elimu katika jimbo hilo, akidai kuwa CCM imemsimamisha mgombea mgeni asiyeijua hali ya wananchi.

“Mbunge wao ni mtalii, hajui hali halisi ya wananchi. Mimi nimeishi Dar es Salaam, nazijua changamoto za Kibamba nje na ndani,” amesema Kinabo.

Kinabo ameahidi Kukabili tatizo la maji, akilenga kupunguza upotevu wa maji kwa zaidi ya asilimia 40, Kuboresha barabara za Kibamba, akirejea kukwama kwa mradi wa DMDP unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

“Tusikubali Kibamba kuwa majaribio ya kisiasa. Nipeni kura nilete heshima ya kweli,” amesema Kinabo kwa kujiamini.