NMB yaahidi kuendeleza ubunifu kwa wateja

Dar es Salaam. Benki ya NMB imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuwa kinara wa huduma bunifu, jumuishi, na zinazokidhi mahitaji halisi ya soko.

Hayo yameelezwa leo wakati wa uzinduzi wa wiki ya huduma kwa wateja yenye kauli mbiu ya “Lengo Linawezekana” (Mission: Possible),” sio kauli tu bali ni ahadi wanayoitekeleza kila siku kama sehemu ya utamaduni wa kuyapa maslahi ya wateja kipaumbele.

Katika risala yake kwenye uzinduzi huo jijini Arusha, Ofisa Mkuu wa Huduma Shirikishi, Nenyuata Mejooli aliyemuwakilisha Ofisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna, alisema, kauli mbiu hiyo inaakisi uhalisia wa mwelekeo mpya wa benki hiyo katika kuwahudumia wateja wake.

“Kauli mbiu ya mwaka huu inaonesha kwamba huduma bora sio ndoto tu bali pia ni dhamira tunayotekeleza kila siku kwa kuwapa wateja wetu thamani halisi,” Ofisa huyo Mkuu wa Huduma Shirikishi aliwaambia wateja waliodhuria hafla hiyo iliyokolezwa na wimbo maalumu wa kuwaenzi wateja waaminifu wa benki hiyo.

Aliongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamezingatia juhudi endelevu za kuboresha huduma kwa njia jumuishi ikiwemo matumizi ya teknolojia, na uwekezaji katika rasilimali watu.

“Kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya NMB inatambua na kuthamini imani kubwa mliyonayo kwetu. Hili linatuchochea kuendelea kuboresha, kuwekeza na kubuni huduma bora zaidi kwa ajili yenu,” Mejooli aliwaambia wateja hao.

Wakati wa maadhimisho ya mwaka jana, NMB ilizindua kampeni kubwa ya huduma chini ya kauli mbiu “Sisi ni Huduma – Tumekupata!”, iliyolenga kuboresha huduma za kibenki kulingana na mahitaji halisi ya wateja.

Mejooli alisema miongoni mwa mafanikio ya mchakato huo ni kuanzishwa kwa huduma ya Jirani, msaidizi wa kidijitali wa NMB anayeendeshwa na akili bandia (AI), ambaye uwezo wake umeboreshwa zaidi mwaka huu.

Majukumu ya Jirani sasa yamepanuka kutoka kujibu maswali ya wateja pekee hadi kuwawezesha kununua bima moja kwa moja kupitia simu zao.

NMB pia imeboresha huduma ya NMB Mkononi, ambayo sasa inaruhusu kununua na kuuza hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, pamoja na uhamisho wa hadi TZS milioni 30 kwa siku.

Marejesho ya mikopo ya papo kwa papo kupitia app hiyo sasa ni hadi miezi mitatu huku wigo wa malipo ya bili ukiongezwa, na wateja kuweza kutengeneza kadi za kidijitali kwa ajili ya manunuzi mtandaoni.

Mejooli amesema NMB pia imeanzisha mifumo ya kudhibiti foleni katika baadhi ya matawi, na kuongeza usambazaji wa mashine za kuweka pesa (CDMs) ili kuwajengea wateja uwezo wa kujihudumia. NMB pia inazingatia kwa umakini mkubwa suala la usalama wa fedha za wateja na taarifa zao.

Mejooli alihitimisha risala yake kwa kuwaalika wateja kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za Wiki ya Huduma kwa Wateja, kutoa maoni yao, na kujifunza zaidi kuhusu mwelekeo mpya wa huduma za benki hiyo.

Naye Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, alisema kuwahudumia wateja kwa ubora na umakini ni jukumu la msingi la benki hiyo.

“NMB itaendelea kujizatiti kuboresha huduma zake kwa kuzingatia mahitaji ya wateja ili kuhakikisha wanapata huduma bora, kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” alifafanua.

Kwa upande wao, wateja kupitia mwakilishi wao, Juliana Olutu, waliipongeza benki hiyo kwa kutanguliza masilahi ya wateja katika shughuli zake na kuitaka kuendelea kuwekeza zaidi katika kuwahudumia.