Unguja. Mgombea urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema Serikali atakayoiunda baada ya kuchaguliwa kuiongoza Zanzibar, itahakikisha chaguzi zote zinafanywa bila kuathiri shughuli nyingine za wananchi.
Sambamba na hilo, amerejea ahadi yake ya kuhakikisha maisha bora kwa wananchi wa visiwa hivyo, akiapa kuondoa tozo, kodi na ushuru katika chakula, ili wananchi wapate lishe bora na kujiimarisha kiuchumi.
Othman ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Oktoba 6, 2025 alipozungumza na wananchi wa Chumbuni, Unguja, visiwani Zanzibar, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais.
Amesema Serikali atakayoiongoza itahakikisha chaguzi zote zitafanyika bila kuathiri shughuli nyingine, amani na utulivu visiwani humo.
“Serikali nitakayoiongoza, tutafanya uchaguzi, mamalishe ataendelea na shughuli zake, anayeenda kazini atapiga kura na kuendelea na kazi yake, hatoguswa mtu, hatoumizwa mtu,” amesema.
Amesema kila mtu atapata haki yake, kwa kuwa chama hicho kinaamini, mtu anapopewa dhamana anapaswa kuwajibika kwa wananchi.
Othman amesema iwapo atachaguliwa, hakutakuwa na kiongozi wa umma, atakayeonyesha jeuri mbele ya wananchi, kwa kuwa anawajibika kwao.
Jambo lingine aliloahidi ni kuhakikisha hakutakuwa na aina yoyote ya hujuma, ama ya wananchi kwa wananchi au Serikali dhidi ya wananchi.
Amerejea ahadi ya kurejesha ustawi wa wananchi katika visiwa hivyo, kwa kuhakikisha kila mmoja anapata chakula cha kutosha na anachokistahili.
“Flyover hailiwi. Sisi tutasimamia ustawi wa watu na ustawi wa mwanzo ni kwenye chakula. Ahadi yetu ni kuondoa kodi, tozo na ada zote kwenye chakula,” amesema.
Othman amesema jukumu lingine atakalolitekeleza ni kuhakikisha wananchi wanapata shughuli zitakazowaingizia kipato, ili kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali atakayoiunda haitawatumikisha watu, badala yake itakuwa inawatumikia wananchi, kwa kuwa ndio wajibu wake.
“Twende tukaunde Serikali tuwatumikie ndugu zangu. Niwaombe mnichague na kuwachagua wawakilishi na wabunge kuondoa manyanyaso kwa wananchi,” amesema Othman.
Awali, akizungumza kumkaribisha Othman, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema wananchi wa Zanzibar hawana budi kumchagua Othman kwa sababu ndiye mwanafunzi sahihi wa Maalim Seif Sharif Hamad.
Maalim Seif (marehemu) alikuwa mwenyekiti wa chama hicho na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, wadhifa aliowahi kuushika pia, alipokuwa mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF).
“Mwanafunzi aliyesoma, akahitimu na akashiba elimu kutoka kwa Maalim Seif naomba waeleze hapa hadharani,” amesema.