Polisi yachunguza madai ya kutekwa kwa Polepole, familia yazungumzia

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limesema linaendelea kufanyia kazi madai ya kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, yaliyotolewa na ndugu zake.

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo, Oktoba 6, 2025, na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime, Polisi imesisitiza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linamsubiri Polepole ajitokeze na kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kama lilivyoelekeza Septemba 15, 2025, wakati lilipotangaza kufungua jalada la uchunguzi kuhusu tuhuma zilizotolewa na mwanasiasa huyo.

Polepole alijiuzulu nafasi ya ubalozi Julai 13, 2025, akieleza kuwa hawezi kuendelea kushiriki katika uongozi usiozingatia utii wa katiba, haki, maadili, utu, na uwajibikaji.

Usiku wa kuamkia Septemba 6, 2025, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinadai kuwa Polepole ametekwa baada ya nyumba yake kuvunjwa na watu wasiojulikana.

Picha mjongeo zilizochapishwa mtandaoni zinaonesha milango na geti la nyumba hiyo vikiwa vimevunjwa, huku damu zikionekana kutapakaa ndani na nje ya nyumba hiyo inayodaiwa kukaliwa na Polepole.

Godfrey Polepole, aliyejitambulisha kama mdogo wa mwanasiasa huyo, akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC leo, Jumatatu Oktoba 6, 2025, amedai kuwa wamekuta nyumba ikiwa imevunjwa na damu zikiwa zimetapakaa ndani.

“Tulipofika, tumekuta nyaya za umeme zimekatwa, mlango wa geti kubwa umevunjwa na ndani kuna damu nyingi. Tulienda kutoa taarifa kituo cha Polisi, hali ni mbaya,” amedai mdogo wake huyo.

Aidha, Agustino Polepole, aliyetambulika kama kaka wa Polepole kupitia picha mjongea iliyosambazwa mtandaoni, amedai mdogo wake ametekwa na kwamba familia inaendelea kufuatilia hali yake.

“Polepole, ambaye mara ya mwisho alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, ametekwa. Tunaendelea kufuatilia na tutatoa taarifa zaidi,” ameeleza.

Kwa mujibu wa ndugu hao, Polepole anadaiwa kuwa na kifaa maalumu mwilini kinachoonyesha amekuwa akihamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine baada ya tukio hilo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa bado linamsubiri Polepole afike Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili kutoa maelezo kuhusu tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii.

 Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Jeshi hilo, Misime, Polisi limeeleza kuwa Polepole alishatumiwa barua ya wito kwa mujibu wa sheria, lakini hadi sasa hajatekeleza agizo hilo.

“Polepole alitumiwa barua ya wito kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili atoe maelezo kuhusiana na tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia mitandao ya kijamii, lakini hadi leo hajatekeleza maelekezo hayo kwa mujibu wa sheria.

“Jeshi la Polisi limeona taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ndugu zake kuwa ametekwa. Tayari tumeanza kufanyia kazi taarifa husika ili kupata ukweli wake,” imeeleza taarifa hiyo.

Wakili Kibatala aingilia kati

Kufuatia sakata hilo, Wakili wa Polepole, Peter Kibatala, kupitia barua aliyoiwasilisha kwa mamlaka husika, ameitaka Serikali kupitia vyombo vya usalama kutumia mbinu zote kuhakikisha usalama wa mteja wake na kutoa taarifa kwa Watanzania na jumuiya ya kimataifa.

“Tutaendelea kutoa taarifa zaidi juu ya suala hili, zikiwemo hatua tunazozichukua kwa kushirikiana na watu na taasisi mbalimbali duniani kote,” amesema Kibatala.

Septemba 15, 2025, Jeshi la Polisi lilitangaza kufungua jalada la uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa na Polepole, likibainisha kuwa baadhi ya madai yake yanaashiria uwepo wa makosa ya kijinai.

“Tuhuma hizo zinahitaji ushahidi wa kuzithibitisha ili zitakapowasilishwa mahakamani hatua za kisheria zichukuliwe. Jeshi limekuwa likifanya jitihada za kumpata Polepole ili atoe maelezo na vielelezo vitakavyosaidia kuthibitisha tuhuma hizo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, Jeshi la Polisi lilimwelekeza Polepole, ambaye pia aliwahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kufika DCI kutoa maelezo yake kuhusu madai anayoyatoa hadharani kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumza baada ya kuitwa, Polepole alisema hatua hiyo ni dalili njema kwamba Jeshi la Polisi limeanza kuchunguza viashiria vya makosa aliyoyabainisha.

“Hili ni jambo jema na huu ni upande mmoja, lakini upande wa pili ni ujanja ujanja. Wanasema wamenitafuta bila mafanikio, lakini kama Polisi hawana namba yangu wangeuliza Wizara ya Mambo ya Nje, wangenipata kwa urahisi. Mimi najibu simu na ujumbe mara nyingi nikiwa kwenye mazingira rafiki,” alisema.

Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa waoga kufuatia hali ya kisiasa, jambo linalompa mashaka makubwa, lakini yeye ataendelea kusema ukweli wake bila woga.