SIKOSELI SI MWISHO WA NDOTO YA UJAUZITO UNAWEZA KUJIFUNGUA SALAMA

Hii ni muhimu kwa wanawake wanaopanga ujauzito, kupima na kujua hali ya mwenza ni hatua muhimu katika kufanya maamuzi ya kupata watoto.

Kabla ya Ujauzito, anaeleza maandalizi muhimu kwa mwanamke mwenye seli mundu, hatua ya kwanza muhimu anashauriwa kumjulisha daktari kuhusu mpango wa kupata mtoto.

Jamila anafafanua kwamba, kupima mwenza wako kama naye ni mbebaji au ana ugonjwa wa seli mundu, kufanya vipimo vya afya kama moyo (ECHO), shinikizo la damu, damu, mkojo na retina ya jicho.

“Kuacha kutumia dawa kama hydroxyurea miezi mitatu kabla ya mimba, kupokea chanjo dhidi ya homa ya ini (Hepatitis B) na nimonia, kuanza kutumia dozi kubwa ya folic acid kila siku.”

Vilevile unaambiwa, matunzo wakati wa ujauzito ni suala la kutofanya ajizi hata kidogo ,hudhuria kliniki mara kwa mara angalau kila wiki 4 hadi wiki ya 24, kisha kila wiki 1 hadi 2 hadi utakapojifungua, pimwa damu na mkojo mara kwa mara.

“Kujifungua kunaweza kuanzishwa wiki ya 38, hasa kama hatari zimeonekana,

katika hatua za uchungu, utapewa oksijeni, dripu ya maji, matunzo ya joto la mwili, kuongezewa damu iwapo una upungufu, ufuatiliaji wa mapigo ya moyo ya mtoto”

Nae Dkt. Pius Muzzazzi, Daktari Bingwa wa Watoto na Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi anaeleza, Ujauzito kwa mama mwenye sikoseli ni safari ya ujasiri, inayohitaji maandalizi, msaada wa kitaalamu na elimu sahihi, kwa matunzo bora, wanawake wengi wenye sikoseli wanaweza kupata watoto wenye afya nzuri bila kuhatarisha maisha yao.

Muzzazzi anaongeza kusema, hakuna madhara ya kunyonyesha ukiwa na seli mundu kwani mtoto anaweza kupimwa kama amerithi jeni za ugonjwa wiki moja baada ya kuzaliwa.

Aidha, Muzzazzi anaeleza, watoto takriban 300,000-400, 000 huzaliwa na sikoseli kila mwaka Duniani, miongoni mwa nchi tano zenye idadi kubwa ya tatizo hilo ni Tanzania ambapo watoto 14,000 huzaliwa na gonjwa hilo kila mwaka, huku vifo asilimia 7 chini kwa watoto walio chini ya miaka mitano.

Mratibu wa huduma ya Selimundu kutoka Wizara ya afya Asteria Mpoto, anahimiza ni muhimu jamii ijenge utamaduni wa kupima kabla ya kuingia katika ndoa au kuanzisha familia ili kupata uelewa sahihi wa hali za kiafya.

Mohamed Abdala Lukemo, kiongozi kutoka Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kata ya Picha ya Ndege, anaeleza alikuwa hajui ugonjwa wa sikoseli ,dalili na athari zake lakini kupitia elimu zinazotolewa kwasasa anaufahamu na atakuwa balozi wa kuelimisha wajukuu, watoto wake, majirani na waumini.