Sumaye: Vurugu haziwezi kuiondoa CCM madarakani

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), hakiwezi kuondoka madarakani kwa upinzani kuchochea fujo na vurugu.

Amesema ili kuiondoa CCM madarakani, kinahitajika chama cha upinzani kinachofanya siasa safi, akibainisha kutumia njia ya kutukana au vurugu, hakuwezi kuiondoa madarakani.

“Hizi fujo zinachochewa na watu wa nje ambao walitamani miaka mingi kuiona CCM inaanguka, lakini wanashindwa, hivyo kulazimika kutumia kikundi cha watu wachache kutukana,” amesema Sumaye.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika leo Jumapili Oktoba 5, 2025, Sumaye amesema: “Wakitaka CCM iondoke sio kuchochea fujo, Watanzania hawataki kusikia kitu kinaitwa fujo, wakitaka wawasaidie hawa ambao ni vyama vya upinzani, wavijenge viwe na uwezo wa kupambana na CCM, sio vyama vya kutukana watu.”

Amesema vyama hivyo havipaswi kufanya kazi za uanaharakati, bali kufanya siasa itakayowashindanisha na chama tawala kwenye sanduku la kura.

“Upinzani ukishinda CCM itakaa pembeni, lakini sio kutaka kuiondoa kwa kutukana matusi au kuchochea vurugu ambazo kimsingi, katika siasa havijengi,” amesisitiza Sumaye.

Amesema Watanzania wanachokihitaji ni kuishi kwa amani na kuwa kitu kimoja.

“Kuna watu wanawatumia watu kuchochea, wakiona Tanzania tunakwenda mbele na kuona baada ya muda hatutaomba misaada kwao, hawapendezwi, wanatamani vurugu zitokee ili wao waendelee kutunyonya.

“Hata hivyo, wamekuta Watanzania tunajielewa, waasisi wetu walitulea vizuri katika misingi ya amani na kuwa nchi ambayo watu wanaitolea macho na kuitamani kutokana na amani tuliyo nayo,” amesema Sumaye.

Amesema amani iliyopo nchini ndiyo inasababisha Tanzania itolewe macho na watu aliosema ni wa nje wanaowatumia baadhi ya watu kutumika kuchochea vurugu kusudi ionekane kuna vurugu wakiamini ndiyo njia ya kuiondoa CCM madarakani.

“Suluhishio sio kutukana, ili kuiondoa CCM ni kuvisaidia vyama vya upinzani viweze kushindana na CCM, hao wanaotaka CCM itoke waanze kuimarisha vyama vya upinzani kwanza.

“Kama watachagua chama kimoja au viwili ili vifanye kazi za siasa na kuvijenga na sio kuchanganya siasa na uanaharakati, hiyo si njia ya kuiondoa CCM,”amesema Sumaye.

Amesema upinzani wa kweli unajengwa katika siasa safi inayoanzia chini kwenye mizizi, kisha chama hicho kinatengeneza ushawishi kwa wananchi na kupata viti vingi vya ubunge kabla ya kutizama nafasi ya urais.

“Ni kama wanavyofanya kule kwao (nchi za magharibi). hawajawahi kufanya uanaharakati kwenye vyama vyao vya vya siasa, hatusikii kuna chama cha siasa kinatengenezwa ili kitukane walioko madarakani. Vyama vyao vinatengenezwa ili kushindana na chama tawala, kwenye uchaguzi, chama tawala kikishindwa kinakaa pembeni, nacho kinajitengeneza ili safari ijayo kirudi kwenye game, ndivyo wanavyofanya, si kufanya siasa za kiuanaharakati na kutukana, hapana,” amesema kiongozi huyo mstaafu.

Amesema Afrika inapaswa kuwa macho, kuhakikisha vyama vinashindana kihalali sio vingine vinaleta vitisho na vingine kuchafua hali ya hewa.

“Kufanya siasa za mabavu haitakiwi, siasa haina mabavu ni ushawishi ambao kama upinzani utaitumia, ndio pekee unaweza kuiondoa CCM.”

Sumaye amedai kwa miaka mingi watu wa nje wanatamani CCM ianguke, tangu wakati wa Tanu, matamanio hayo yalikuwepo.

“Tangu enzi ya Mwalimu (Baba wa Taifa) watu wa nje walitamani Tanu ianguke, lakini haikuanguka, ilipoungana na Afro Shiraz ikawa imara zaidi na kuzaliwa CCM, wamekuwa wakitamani ianguke, lakini wanaona nchi ina maendeleo na utulivu, wao hayo hayawapendezi.

“Nchi za Afrika zikichafuka hao hao ndio wanaokuja kuinyonya kwa madai kwamba wanaisaidia, ndiyo maana vita vya wenyewe kwa wenyewe Afrika haviishi, hao wakubwa watagawana nchi, wengine watasaidia upande wa Serikali na wengine watasaidia upande unaopigana na Serikali, wote lengo ni kuinyonya hiyo nchi,” amesema.

Akizungumzia hali ya sintofahamu iliyopo hivi sasa, Sumaye amesema katika hali ya kawaida mtu mwenye akili hawezi kuamka tu na kuanza kumtukana kiongozi wa nchi.

“Lazima kuna nguvu fulani inayokwambia wewe sema hivi mimi nipo nyuma yako, hao watu wapo miaka yote tangu wakati wa Mwalimu, lugha mbaya zilikuwepo kwa watu wa aina hiyo.

“Nakumbuka wakati ule wa ujamaa, kuna watu waliibuka na kusema huyu bwana (Mwalimu) ametutelekeza ametuletea mabaya, lakini ni kundi la watu wachache, ila walio wengi wanajua mzee Nyerere alikuwa anatuelekeza kwenye neema ya baadaye,” amesema Sumaye.

Amesema alipoingia madarakani Rais Ali Hassan Mwinyi, mambo yalikuwa ni hayo hayo, alisemwa sana hadi watu wakasema labda kwa vile ni Mzanzibari au Muislamu.

“Vivyo hivyo wakati wa Rais Benjamini Mkapa, naye alisemwa sana,  akaja ndugu yetu Kikwete (Jakaya Mrisho) huyu alisemwa sana sambamba na familia yake.

“Lakini tunajua vilikuwa ni vita ambavyo si vya Kikwete na familia yake, ilikuwa ni vita vya CCM, hivi sasa Rais ni Samia (Suluhu Hassan), miaka yote kumekuwa na jambo hilo, lakini wanaozungumza kuna watu nyuma yao,” amesema.

Akigusia miaka kadhaa iliyopita alipoondoka CCM na kuhamia upinzani, Sumaye amesema, “katika hotuba yangu nilisema sina ugomvi na CCM, sina ugomvi na mteule wake (mgombea urais wa wakati huo) sina ugomvi na mwenyekiti, ambaye wakati ule alikuwa ni Rais Kikwete.

“Nilisema natamani Tanzania angalau tuwe na vyama viwili vinavyoshindana kwa haki,

hali hiyo ikifikiwa tutakuwa na maendeleo mazuri kwa sababu kila chama kitajitahidi kwa sababu kinaona kuna mwenzake anapiga indiketa.”

Amesema alipohamia upinzani, alijitahidi kuwaelewesha hilo, lakini  hawakuelewa badala yake yeye ndiye alipata matatizo.

“Niliporudi CCM nilisema hivi, nimetoka upinzani nimerudi, naamini CCM  inahitaji chama kizuri cha upinzani katika nchi hii, nikasema lakini kwa vyama vilivyopo sioni kinachoweza kufanya hiyo kazi.

“Vingi vina  ubinafsi ama vina uanaharakati, lazima kipatikane chama kitachokomaa katika ustaarabu wa siasa ili kijienge nguvu, Watanzania wanufaike, bado naamini hivyo,” amesema.

Amesema kwa vyama vilivyopo, haoni chenye muelekeo huo, akibainisha ili chama kijijenge kuna mambo mengi, kwanza ni chenyewe kuwa na demokrasia ya kweli na si kuwa na ubinafsi.

“Demokrasia ya kweli ni kuruhusu ushindani ndani ya chama chenyewe bila kuleta chuki, pia chama kiwe na ushawishi wa kweli kwa Watanzania.

“Hauwezi  kutengeza ushawishi wa kweli kwa kwenda kutukana nchi au kubeza shughuli zinazofanywa na Serikali kwa sababu tu ni ya CCM,”amesema.

“Fanya siasa safi ili wananchi wakuone, wenyewe watasema huyu mtu anakubaliana na haya, lakini kama ingefanyika hivi ingekuwa vizuri zaidi, hivyo watasema ngoja tumjaribu huyu na si kwa kutukana au kuanzisha fujo,” amesema.

Amesema wananchi hawatakujaribu kwenye urais mara ya kwanza, akibainisha chama chochote cha siasa kinaanza kwa kuweka nguvu kubwa ndani ya Bunge.

“Ukiwa na timu kubwa, haiwezi kuwa majority, wabunge wako watakavyokuwa wanajenga hoja na ku-challenge  yale maeneo yenye kasoro,  ndivyo wananchi wataanza kukupenda  na wakikupenda basi chama kitajenga mizizi.

“Lakini vyama vingi nchini, hata kabla wananchi hawajaanza kukupenda, chama hakijaanza kujijenga watu wanapigania kiti cha urais, unashindaje urais wakati ujajenga mizizi huko chini?,” amehoji.

Amesema katika upinzani, ili kuiondoa CCM kuna kazi kubwa inayotakiwa ifanyike, kwani CCM iko mbele sana, akisema ili kuiondoa si kuangalia kutaka kuivuta nyuma, ni kutafuta namna ya kukaza mbio ili uikute.

Mahojiano zaidi na Sumaye kuhusu mwenendo wa kampeni, endelea kufuatilia Mwanachi