TEF Yalaani Vikali Wito wa Wanajeshi Kujihusisha na Siasa – Global Publishers

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limelaani vikali kauli na maudhui yaliyosambazwa katika mitandao ya kijamii Oktoba 4, 2025, yakionesha watu wanaodaiwa kuwa wanajeshi wakihamasisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiingiza katika siasa kupitia mapinduzi.

TEF imesema hatua hiyo ni hatari kwa amani ya nchi, uthabiti wa demokrasia na misingi ya kitaifa iliyoijenga Tanzania tangu uhuru, ikionya kuwa hoja kama hizo zinaweza kuathiri umoja wa Taifa na kuharibu taswira ya Jeshi linaloaminika barani Afrika.

Katika taarifa iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF tarehe 5 Oktoba 2025, Deodatus Balile, Jukwaa hilo limepongeza uamuzi wa haraka wa JWTZ kutoa taarifa ya kukanusha na kukemea vikali majaribio ya kulihusisha Jeshi na siasa, likinukuu sehemu ya taarifa hiyo ikisema:

“JWTZ inapenda kuutaarifu umma wa Watanzania, kuwa inaendelea kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa uaminifu, utii na uhodari kwa kuzingatia kiapo chetu.”

TEF imekumbusha kuwa tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Tanzania imekuwa mfano wa demokrasia ya amani, huku chaguzi zikiendelea kufanyika kwa utulivu na wananchi wakiamua viongozi wao kupitia sanduku la kura si kwa mapinduzi.

“Tanzania ilijaribiwa mapinduzi mwaka 1964, 1969 na 1982, lakini kwa hekima ya viongozi na umoja wa wananchi, nchi yetu ilishinda majaribu hayo na kujenga mfumo thabiti unaotenganisha Jeshi na siasa. Wanajeshi wa Tanzania hawaruhusiwi kuwa wanachama wa vyama vya siasa msingi huu ndiyo ngao ya amani na utulivu wetu”, imesema taarifa hiyo.

TEF imeonya kuwa kauli za uchochezi dhidi ya Jeshi ni hatari na zinavunja misingi ya Taifa, ikitoa wito kwa vyama vya siasa, wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kuzisambaza au kuzitumia kama nyenzo za kisiasa.

“Vyama vya siasa navyo visikalie kimya kauli zenye mwelekeo wa uchochezi. Kila chama kinapaswa kujitenga na matamko hayo kwa kuyalaani bila woga, kwa nia ya kulinda umoja, maisha na mali za watu wetu. Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja na mshikamano. Njia pekee ya kuendeleza uongozi ni kupitia demokrasia na ridhaa ya wananchi”, imeeleza taarifa hiyo.