TISEZA YALETA UPEPO MPYA KATIKA UWEKEZAJI, MIRADI YA DOLA MILIONI 2,538 YASAJILIWA KWA ROBO YA KWANZA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji, Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (TISEZA) Gilead Teri,akionesha bango la mafanikio ya uwekezaji wakati akitoa taarifa ya uwekezaji kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026.Jijini Dar es Salaam leo Oktoba 06, 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji, Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (TISEZA) Gilead Teri,akizungumza leo Oktoba 06, 2025 jijini Dar es Saaam wakati akitoa taarifa ya uwekezaji kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Na Avila Kakingo, Michuzi Tv

SEKTA ya uwekezaji nchini Tanzania inaendelea kushuhudia mwamko mpya wa kasi, ufanisi na matumaini, kufuatia jitihada za Mamlaka ya Uwekezaji, Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (TISEZA) katika kusimamia na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai–Septemba 2025), TISEZA imesajili jumla ya miradi 201 yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 2,538.56 za Marekani, sawa na shilingi trilioni 6.18 za Kitanzania, ikitarajiwa kuleta ajira zaidi ya 20,800 kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 06, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, wakati akitoa taarifa ya uwekezaji kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 amesema kuwa hii ni hatua kubwa na ya kihistoria ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (TIC) ilisajili miradi 256 kwa mwaka mzima.

“Matokeo haya yanaonyesha mabadiliko makubwa katika ufanisi wa usajili wa miradi, hasa katika kipindi hiki cha mpito cha kuunganisha taasisi za uwekezaji chini ya mwamvuli mmoja wa TISEZA.” Amesema Teri

Amesema moja ya mafanikio makubwa katika kipindi hiki ni ongezeko la miradi ya uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya mauzo ya nje (EPZ). “

TISEZA imesajili miradi minane (8) yenye thamani ya dola milioni 97.83, ikitarajiwa kutoa ajira kwa zaidi ya watu 2,600 na kuingiza nchi mapato ya fedha za kigeni ya takribani dola milioni 127.53.

Ikilinganishwa na miradi mitatu tu iliyosajiliwa mwaka uliopita, ongezeko hili linaashiria kuimarika kwa mazingira ya biashara na kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika soko la Tanzania.”

Akizungumzia ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji Teri amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa miradi inayomilikiwa na Watanzania imeongezeka kutoka 70 mwaka 2024/25 hadi 74 katika robo ya kwanza pekee ya mwaka huu ongezeko la asilimia 5.7.

“Hii inaonyesha mwamko mpya wa wananchi kujitokeza kuwekeza katika sekta mbalimbali, ishara ya kuongezeka kwa uelewa na imani kwa sera za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Ameeleza

Pia ametaja sekta zinazoongoza kiuchumi kuwa ni sekta ya viwanda ambayo imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa usajili wa miradi mipya, ikiwa na miradi 85 sawa na asilimia 42.29, ikifuatiwa na ujenzi wa majengo ya biashara (miradi 30, 14.93%) na usafirishaji (miradi 29, 14.43%).

Kwa upande wa mikoa iliyoongoza kwa usajiri wa miradi kuwa ni Dar es Salaam ambayo imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji nchini kwa kuwa na miradi 79 (39.3%), ikifuatiwa na Pwani (miradi 29) na Arusha (miradi 16).

Akizungumzia Wawekezaji wakubwa wanaoongoza kwa mitaji Teri amesema wanatoka katika Falme za Kiarabu (UAE), China, na India, wakichangia jumla ya zaidi ya asilimia 68 ya thamani yote ya uwekezaji mpya.

Jitihada za TISEZA kuendelea kutangaza uwekezaji nchini imezindua kampeni maalum ya kuvutia uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs), ikilenga maeneo matano ya kimkakati: Bagamoyo, Kwala, Benjamini Mkapa–Mabibo, Nala na Buzwagi.

Kupitia kampeni hii, mamlaka inalenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta za uzalishaji, huku Watanzania wakihamasishwa kushiriki kwa umiliki wa asilimia 100 au kupitia ubia wa angalau asilimia 30.

Teri ametaja Sekta kumi (10) zimepewa kipaumbele maalum, zikiwemo, Bidhaa za matumizi ya haraka (FMCG), nguo, dawa, magari na vipuri vyake, bidhaa za karatasi na vifaa vya ufungaji, teknolojia za nishati jadidifu, samani na vifaa vya ujenzi.

“Kipaumbele hiki kinaendana na ajenda ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda unaotumia teknolojia na ubunifu wa ndani.”

Serikali Yazidi Kuweka Mazingira Rafiki wa mujibu wa TISEZA, mafanikio haya ni matokeo ya sera thabiti za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya viwanda, ubunifu na teknolojia.

Kupitia mabadiliko hayo, Tanzania inajitokeza kama kitovu kipya cha uwekezaji Afrika Mashariki, chenye sera rafiki, miundombinu inayoimarika, na nguvu kazi kubwa ya vijana.

TISEZA inatoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hizi za uwekezaji, kushiriki katika miradi ya uzalishaji, na kuwa sehemu ya ajenda ya taifa ya uchumi wa viwanda.

Kwa kiwango cha miradi kilichosajiliwa ndani ya miezi mitatu pekee, TISEZA imeonyesha uwezo mkubwa wa kuongoza mageuzi ya uwekezaji nchini. Hatua hii inaiweka Tanzania kwenye ramani ya Afrika kama taifa lenye mazingira thabiti, rafiki na endelevu kwa wawekezaji.

Ni dhahiri, dira ya uwekezaji wa kisasa inayosimamiwa na TISEZA inalenga si tu kuvutia mitaji, bali kujenga Tanzania yenye uchumi imara, shindani na jumuishi