TTCL YAHAKIKISHIA HUDUMA BORA KWA WATANZANIA WOTE


 ::::::::::::

Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema litaendelea kuwekeza katika teknolojia za
kisasa, kuboresha mifumo yao, na kuhakikisha huduma bora zinawafikia Watanzania
wote popote walipo ili kuhakikisha
kila mwananchi ananufaika na maendeleo ya mawasiliano nchini.

Kauli hiyo imetolewa
na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TTCL, Bi. Anita Moshi, wakati wa uzinduzi
wa Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025 iliofanyika  mapema 
leo Oktoba 6, jijini Dar es Salaam.

Bi Moshi  Alisema maadhimisho hayo ni fursa ya
kutathmini utoaji wa huduma kwa wateja na kuimarisha uhusiano wa karibu kati ya
shirika na wananchi.

 alieleza kuwa ujenzi wa minara 1,400 ya
mawasiliano
katika maeneo ya vijijini unaendelea kwa kasi, ikiwa ni sehemu
ya jitihada za kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za mawasiliano bila
kikwazo, hasa katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na changamoto za
upatikanaji wa huduma hizo.

Sambamba na hilo
shirika  linaendelea kutekeleza mpango wa
upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo
kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi kufikia wilaya zote za
Tanzania.

 Mpango huo ni msingi wa kuhakikisha huduma za
intaneti na mawasiliano ya sauti zinaimarika hadi ngazi ya jamii.

Kupitia huduma ya “Faiba
Mlangoni Kwako,” TTCL inaleta huduma ya intaneti yenye kasi, uhakika na
viwango vya kimataifa kwa Watanzania mijini na vijijini. Bi. Moshi alisema
huduma hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali,
elimu mtandaoni, na huduma za kijamii.

Maadhimisho ya mwaka
huu yamebebwa na kaulimbiu “Mission: Possible,” ambayo inalenga kuhimiza
ubunifu, mshikamano na utayari wa kutatua changamoto katika kutoa huduma bora
kwa wateja. Bi. Moshi alisisitiza kuwa kila mfanyakazi wa TTCL ni sehemu ya
suluhisho na mafanikio ya shirika.

Aidha, amewasihi
wateja  kuendelee kutumia vituo vya
huduma kwa wateja vinavyopatikana saa 24, pamoja na maduka ya TTCL na mitandao
ya kijamii kwa ajili ya kupata huduma na kutoa mrejesho. Alisema shirika
linasikiliza na kufanyia kazi maoni ya wateja ili kuendelea kuboresha huduma
zake.

Akihitimisha, Bi.
Moshi alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuiamini TTCL na kushiriki
kikamilifu katika Wiki ya Huduma kwa Wateja. Alitangaza rasmi uzinduzi wa wiki
hiyo kwa mwaka 2025 na kusisitiza kuwa shirika litaendelea kuwa bega kwa bega
na wananchi katika safari ya kujenga taifa la kidijitali.

                                        

                              PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCHMEDIA