::::::::::
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetangaza ongezeko kubwa la uwekezaji nchini katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, hali inayoashiria mwitikio chanya kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 6, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, alisema jumla ya miradi 201 imesajiliwa katika kipindi hicho, yenye thamani ya shilingi trilioni 6.18 na matarajio ya kuzalisha ajira 20,808 kwa Watanzania.
“Hizi ni takwimu ambazo zinatia moyo na tunawapongeza wawekezaji wetu wa nje na wa ndani kwa imani yao katika mazingira ya uwekezaji hapa nchini,” alisema Teri.
Teri alibainisha kuwa mafanikio hayo yanadhihirisha ufanisi wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Aidha, alisema mwitikio huo umeonyesha mafanikio makubwa ukilinganisha na mwaka 2021 ambapo, wakati huo mamlaka ilikuwa chini ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), miradi 256 ilisajiliwa kwa mwaka mzima.
Katika hatua nyingine, Teri alisema kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji, ambapo miradi inayomilikiwa na Watanzania imeongezeka kutoka 70 hadi 74, sawa na ongezeko la asilimia 5.7.
“Tunajivunia kuona Watanzania nao wakijitokeza zaidi katika uwekezaji. Hili ni jambo la kutia moyo na ni kielelezo cha mwamko unaoendelea kujengeka miongoni mwa wazawa,” aliongeza.
TISEZA inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuboresha zaidi huduma kwa wawekezaji kwa lengo la kuongeza ushindani wa Tanzania katika kuvutia mitaji mipya ya ndani na ya kimataifa.