Unguja. Licha ya matumbawe kuwa rasilimali muhimu, yanatajwa kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kukosa uelewa wa namna ya kuyalinda na kuyahifadhi, kukosekana kwa mifumo na miundombinu ya mpango wa kitaifa na ukosefu wa fedha wa kuendeleza rasilimali hiyo.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Taasisi ya bahari na maeneo tengefu Tanzania (MPRU) kwa kushirikiana na idara ya uhifadhi wa bahari kutoka Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, wameandaa mradi maalumu wa hifadhi ya matumbawe (CRRI) utakaotekelezwa kwa miaka minne.
Mradi huo unaofadhiliwa na Global Environment Facility (GEF) na unafanya kazi katika nchi sita ikiwemo Fiji, Indonesia, Madagascar, Ufilipino, Visiwa vya Solomon na Tanzania, una lengo la kuhifadhi rasilimali hiyo kwa masilahi ya jamii.
Melanie Johnson kutoka Chuo Kikuu cha Queensland nchini uingereza akiwasilisha mada katika kikao cha kuwajengea uwezo wadau wa uhifadhi ya bahari kilichofanyika Mjini Unguja. Picha na Zuleikha Fatawi
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Oktoba 6, 2025 na mratibu wa mradi huo, Godfrey Ngupula katika kikao cha kuwajengea uwezo wadau wa uhifadhi ya bahari kilichofanyika Mjini Unguja.
“Changamoto kubwa inayoikumba rasilimali hiyo ni watu kutokuwa na uelewa kwa kuyavamia matumbawe kwa kasi hasa wavuvi wanaotumia nyavu haramu,” amesema Ngupula.
Amefafanua kuwa katika kudhibiti hilo, ndio sababu ya kushirikiana na Serikali kupiga vita uvuvi huo, ili kuwafanya wananchi kutokuwa maadui na rasilimali zenye kuleta faida kwao.
Amesema kutokana na miundombinu iliyowekwa katika matumbawe, wanaamini kuwa hayatakuwa katika hatari ya kutokewa kwa namna yanavyodhibitiwa.
Amesema athari mojawapo inayotokana na kutoweka kwa matumbawe ni kupotea kwa uvuvi kwani mazalia ya samaki yanatokana na rasilimali hiyo.
Naye, msimamizi mkuu wa mradi huo kwa upande wa Zanzibar, Yassir Ali Haji amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha matumbawe yanalindwa kwani yana uhimilivu mkubwa.
Pia, amesema mradi huo umetoa fursa kwa jamii kujifunza kozi mbalimbali kupitia Chuo Kikuu cha Queensland cha nchini Uingereza kwa kupata cheti kinachoweza kumsaidia kutambulika kuwa msimamizi wa matumbawe.
Amesema chuo hicho kimekuja na mradi huo unaotekelezwa katika nchi sita baada ya kugundua nchi hizo matumbawe yake yana uhimilivu mkubwa, katika uzalishaji wa samaki na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Queensland, Melanie Johnson amesema katika utafiti ulioongozwa na chuo hicho na zaidi ya washiriki 20 wa uhifadhi, uligundua kuwa baadhi ya miamba ina athirika kutokana mabadiliko ya hali ya hewa katika eneo la bahari kama vile mikondo na kuongezeka kwa maji.
Amesema mradi huo unalenga kujenga uwezo, ushiriki wa habari na masuluhisho ambayo yanahakikisha uhai wa muda mrefu wa mifumo ikolojia ya matumbawe, kuhifadhi bayoanuwai yao na kusaidia uchumi wa buluu na jamii zinazoitegemea.
“Mradi huu unachangia mpango wa kimataifa ili kulinda afya ya mifumo ya ikolojia ya miamba ya matumbawe licha ya matishio ya hali ya hewa,” amesema Melanie.