Wanachama wa ACT Wazalendo Konde wajiunga na CCM

Pemba. Wanachama hao wamerejesha kadi zao na kujiunga na CCM leo Oktoba 6, 2025 katika mkutano wa kampeni za mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa Msuka, alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama hao, Naima Ali Abdallah amesema wameamua kujiunga na CCM kutokana na maendeleo ambayo yamefanywa na chama hicho.

“Tumekuwa tukidanganywa kule tulipokuwa, kwa hiyo tumeamua kuja kujiunga na CCM maana yanayofanyika yanaonekana waziwazi,” amesema.

Akiwatambulisha wanachama hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa amesema wanachama hao bila kushawishiwa na mtu yeyote, wameamua kwa hiari yao kujiunga na chama hicho.

“Mheshimiwa mgombea wetu, tunataka tukupe zawadi, hawa wanachama walikuwa ACT Wazalendo, kwa idadi yao ni 364, wameamua wenyewe kujiunga na chama chetu,” amesema Dk Dimwa.

Akiwakaribisha wanachama hao, Dk Mwinyi amewapongeza kufanya uamuzi sahihi kujiunga na chama hicho.

“Mmefanya uamuzi sahihi kujiunga CCM, karibuni ninawapongeza sana,” amesema Dk Mwinyi.