Wateja wapongeza Mageuzi ya Mfumo Benki ya CRDB ikisherehekea Wiki ya Huduma kwa Wateja

 

Dar es Salaam. Tarehe 06 Oktoba 2025: Benki ya CRDB leo imezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025 katika hafla iliyofanyika katika tawi la Dar Village jijini Dar es Salaam, ikiambatana na kaulimbiu ya kimataifa ya “Mission Possible” ambayo Benki hiyo imeitafsiri kama “Mkakati Unaowezekana.”

Uzinduzi huo uliohudhuriwa na wateja, wafanyakazi, wadau wa sekta ya fedha, na waandishi wa habari, uliongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bank, Boma Raballa, ambaye alisisitiza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inaakisi safari ya mafanikio ya miaka 30 ya Benki hiyo, safari iliyojengwa juu ya uthubutu, ubunifu, na uhusiano wa karibu na wateja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Raballa alisema historia ya Benki ya CRDB inathibitisha kuwa “hakuna lisilowezekana” pale ambapo kuna mkakati sahihi na dhamira ya pamoja. “Tulipoanza safari yetu mwaka 1996, wengi walidhani hatutaweza kushindana na mabenki makubwa ya kimataifa. Lakini leo, baada ya miaka 30, Benki ya CRDB ni benki kubwa zaidi nchini Tanzania na kinara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema Raballa.

Alitaja baadhi ya mafanikio makubwa yaliyotokana na uthubutu wa Benki hiyo kuwa ni pamoja na upanuzi wa kimataifa kupitia kampuni tanzu za Burundi na Kongo (DRC), uanzishwaji wa taasisi mpya kama CRDB Insurance na CRDB Bank Foundation, pamoja na ujumuishi wa huduma za kifedha unaowezesha Watanzania kupata huduma za kibenki kupitia mitandao ya mawakala wa CRDB Wakala na mifumo ya kidijitali kama SimBanking.

“Leo hii, mkulima wa parachichi kijijini Madeke mkoani Njombe anaweza kupata huduma kupitia AMCOS yake inayotoa huduma za CRDB Wakala; mwalimu kutoka wilaya ya Malinyi anaweza kutazama mshahara wake kupitia SimBanking bila kusafiri umbali mrefu kwenda tawini; na mama mjasiriamali wa Mwanjelwa anaweza kupata mtaji kupitia program ya IMBEJU bila dhamana yeyote. Hizi ndizo simulizi za Mission Possible,” aliongeza Raballa akionyesha Benki ya CRDB ilikuwa ya kwanza katika kubuni huduma zote hizo kurahisisha huduma kwa wateja.

Raballa alifafanua kuwa mageuzi ya kiteknolojia yamekuwa sehemu ya msingi wa mafanikio hayo. Hivi karibuni Benki hiyo imekamilisha mageuzi makubwa ya kihistoria kwa kuingiza mfumo mkuu mpya wenye viwango vya kimataifa wa Temenos Transact (T24), unaoiweka Benki ya CRDB katika kiwango sawa na mabenki makubwa duniani duniani.

“Mfumo huu umeongeza kasi, usalama na ubunifu wa huduma zetu, ukiwezesha matumizi ya akili mnemba na kujihudumia kwa wateja Pia, umefungua fursa ya kupanua huduma zetu katika masoko mapya kama Dubai,” alisema.

Aliitumia fursa hiyo pia kuwaomba radhi wateja waliopata changamoto wakati wa kipindi cha mpito, akisisitiza kuwa huduma sasa zimerejea katika ubora wake na Benki inaendelea kuboresha mifumo kwa ustahimilivu na kujituma. “Maboresho makubw kama haya hayakosi changamoto. Tunawashukuru wayeja wetu kwa uvumilivu wao na tunawaahidi huduma bora zaidi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo, alisema CRDB Bank inaamini kuwa huduma bora kwa wateja si jambo la msimu bali ni dhamira ya kila siku. “Wiki hii ni fursa ya kuwasherehekea wateja wetu ambao wametupa imani na maoni yanayotuongoza kuboresha huduma kila siku. Pia ni wakati wa kuwapongeza wafanyakazi wetu wanaoishi falsafa ya huduma bora kwa weledi na ubunifu,” alisema.

Uriyo aliongeza kuwa shughuli mbalimbali zimepangwa katika wiki hii, zikiwemo mikutano na wateja, semina, na kampeni za kupokea maoni kupitia majukwaa ya kidijitali.

Akizungumza kwa niaba ya wateja, Hashim Lema aliyekuwa mgeni maalum wa hafla hiyo alitoa pongezi kwa Benki ya CRDB kwa huduma zenye ubunifu, mageuzi ya kidijitali, na ushirikiano wa karibu na wateja wake.

“Benki ya CRDB ni alama ya mafanikio ya kizalendo. Huduma zake zimetusaidia wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima, wanafunzi na wastaafu kutimiza ndoto zetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya Mission Possible,” alisema mteja huyo.