Paris. Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa, Sebastien Lecornu na serikali yake wamejiuzulu saa chache baada ya kutangaza safu yake ya Baraza la Mawaziri, hivyo kuifanya kuwa Serikali ya muda mfupi zaidi katika historia ya Ufaransa.
Serikali hiyo imetangaza kujiuzulu baada ya kukaa madarakani kwa takribani saa 14 tangu kutangazwa na Waziri Mkuu huyo aliyeteuliwa na Rais Emanueli Macron wiki chache zilizopita, kufuatia maandamano yaliyoondoka na kibarua cha mtangulizi wake.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu huyo, imeeleza kuwa mawaziri hao waliteuliwa Jumapili iliyopita na walipanga kufanya mkutano wao wa kwanza Jumatatu alasiri.
Lakini Jumatatu asubuhi, Lecornu alikabidhi barua yake ya kujiuzulu pamoja na baraza lake lote la mawaziri kwa Macron, hatua hiyo ikielezwa kuwa ni baada ya uteuzi huo kuwakasirisha wapinzani na washirika ambao waliona kuwa halitoshi kumaliza matatizo yaliopo ndani ya taifa hilo kwa sasa.
“Sebastien Lecornu amewasilisha barua kujiuzulu kwa serikali yake kwa Rais wa Jamhuri, ambaye amekubali,” imeeleza ofisi hiyo.
Kujiuzulu huko kunatarajiwa kuzidisha mzozo wa kisiasa ndani ya Ufaransa na kuongeza nguvu kwa upinzani ambao tayari ulionyesha nia ya kuipindua serikali ya sasa.
Serikali hiyo imelalamikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa imeshindwa kumaliza matatizo ya kijamii katika sekta za afya na kusababisha kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Kiongozi wa kitaifa, Jordan Bardella ameonyesha wasiwasi wake juu ya kuendelea kwa utawala wa kiongozi huyo, kutokana na uungwaji mkono mdogo kutoka kwa wananchi na washirika wake wa karibu.
Lakini pia kukosekana kwa utulivu kwenye siasa za Ufaransa ambazo zimekuwa zikiyumba tangu kuchaguliwa tena kwa Macron mwaka 2022, ambaye amekosa chochote kinachoshikilia wabunge wengi.
Jambo hilo limeungwa mkono na Mathilde Panot wa chama cha mrengo wa kushoto cha Ufaransa, Unbowed, ambaye amesema kujiuzulu kwa Lecornu pekee hakutoshi, hivyo Macron pia anatakiwa kuondoka.