Uganda. Mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Aisha Masibu mkazi wa Nabuyonga nchini Uganda ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani, wakati akijaribu kuzuia ugomvi uliokuwa ukimuhusisha mume wake.
Tukio hilo lilitokea jana Jumatatu Oktoba 6, 2025 katika eneo la Kikindu, ambako marehemu alikuwa akifanya biashara ya kuuza bidhaa sokoni.
Kwa mujibu wa mashuhuda walionukuliwa na tovuti ya habari ya Daily Monitor , Aisha alijeruhiwa vibaya baada ya kuingilia kati ugomvi huo, kumtuliza mume wake ambaye ni mlinzi wa eneo la maegesho ya magari, wakati alipokuwa akigombana na vijana wawili waliodaiwa kuwa na deni la Shilingi 2,000 (ya Uganda) kwa mteja wa sehemu hiyo.
“Mume wa marehemu alijaribu kuwazuia vijana hao kuingia ndani bila ruhusa, wakaanza kumpiga. Aisha alipokuja kumtetea, walimpiga jiwe kichwani na kuanguka chini akiwa hajitambui,” alisema Ismail Gidudu, dereva bodaboda aliyeshuhudia tukio hilo wakati akizungumza na Daily Monitor.
Baada ya tukio hilo, inadaiwa watuhumiwa hao, wenye umri wa kati ya miaka 19 na 24, walikimbilia nyumbani kwao katika eneo la Kisenyi, Kata ya Nabuyonga, huku mlinzi ambaye ni mume wa marehemu akiachwa na majeraha makubwa.
Kwa mujibu wa Daily Monitor, Msemaji wa Polisi wa Kanda, Rogers Taitika amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji.
Polisi wamesema mtuhumiwa mkuu, anayefahamika kwa jina la Yusuf maarufu kama Fifty Fifty, ni mhalifu sugu ambaye hivi karibuni aliachiliwa kutoka gerezani baada ya kutumikia kifungo cha miezi sita.
Katibu wa Usalama wa Kata ya Nabuyonga, Seku Abdulkarim, amesema Yusuf alianza tena vitendo vya uhalifu baada tu ya kutoka gerezani.
Kwa upande wake, Ofisa Tawala wa Mbale, Hussein Kadimba, amewataka wazazi kuwalea vizuri watoto wao na kufuatilia mienendo yao, akibainisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya yamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la uhalifu miongoni mwao.
Mwili wa marehemu Aisha Masibu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mbale kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.