Maadhimisho Bank of Africa -Tanzania yamewalenga waliofanikisha kuleta mabadiliko chanya – wateja, wafanyakazi na wabia – wanaowezesha kuwa na ubunifu unaofanikisha kutoa huduma bora. Kupitia maadhimisho hayo benki inatambua jitihada za wafanyakazi wake wanaofanya kazi kwa weredi na bidii kufanikisha mabadiliko ya kuhudumia wateja ili kuendana na mfumo wa huduma za kisasa zinazotolewa na benki hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa – Tanzania, Wasia Mushi alisema: “Huduma kwa wateja ni moyo katika uendeshaji wa huduma zetu. Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu ya ‘Dhamira: Inawezekana’ tunathibitisha kujitolea kwetu zaidi ya matarajio, kwendana na mahitaji ya wateja, na kuwa wabunifu kwa kujenga utamaduni wa kuambua kuwa mteja ni wa kwanza katika biashara yetu.” Alisema mkakati wa Bank of Africa -Tanzania kufanya mabadiliko chanya unadhihirisha kwamba jukumu lao siyo tu kwamba upo katika huduma za kifedha, bali pia katika kujenga mustakabali endelevu wa kesho iliyo bora.
Mushi alisema kwamba mwaka huu Bank of Africa -Tanzania imeshuhudia ukuaji mkubwa katika utumiaji wa mifumo yake ya huduma kwa njia ya kidijitali, ikionyesha dhamira yao ya kurahisisha, kupatikana na ubunifu wa huduma za kibenki.
“Tumepanua wigo wa upatikanaji wa huduma kupitia mawakala na mtandao wa mawakala wetu wanaotoa huduma za BOA Lipa, wanawezesha wateja kufanya miamala kwa urahisi nchini kote,” alisema Mushi.
Alieleza kwamba sambamba na lengo lao la kuwawezesha wateja wao, wanajivunia kuanzisha Kadi ya Visa ya Dhahabu ya Dola ya Marekani (Visa Gold USD Card) inayowezesha kufanya manunuzi na kurahisisha matumizi kwa mahitaji binafsi na ya kibiashara.
Mwaka huu, Bank of Africa -Tanzania imetunukiwa tuzo ya ubora wa Usalama wa Data za Kadi ya Malipo (PCI DSS), inayotambulika kimataifa kwa kulinda usalama wa taarifa za wateja wanaotumia kadi na usalama wa mihamala kwa njia za kieletroniki.
Hatua hii muhimu inaonyesha dhamira thabiti ya Bank of Africa -Tanzania ya kulinda taarifa za wateja, kudumisha uzingatiaji wa viwango, na kuendeleza upatikanaji wa huduma salama za benki kwa njia ya kidijitali kote Tanzania.
“Kujitolea kwetu kutoa elimu ya kifedha na uwajibikaji kwa jamii kuko imara Kupitia programu zilizolengwa, tumefanikisha kuleta mabadiliko chanya kwa maelfu ya Watanzania, tukiwapa maarifa kuhusiana na matumizi ya fedha kwa ufanisi na kuwawezesha. Tukiangalia mbeleni, mpango mkakati wetu wa miaka mitatu unalenga kupanua mipango hii zaidi, hasa kwa jamii ambazo hazijafikiwa na huduma za kifedha, na kuhakikisha ushirikishwaji wa kifedha kwa wote.”
Ili kutimiza juhudi hizi, Bank of Africa -Tanzania inaendelea kuboresha Programu ya B-Mobile na jukwaa la BOAWeb, na kuzifanya ziwe na viwango vya juu na rahisi kutumika ili wateja wake waweze kufurahia matumizi ya kidijitali ya kibenki wakati wowote, na mahali popote.
“Tunajivunia timu yetu yenye ari isiyoyumba katika kutoa huduma za kipekee kila siku. Mwezi na Wiki hii ya Huduma kwa Wateja hutupatia fursa nzuri ya kusherehekea kujitolea kwao katika kufanikisha dhamira yetu. Tunafurahi vile kuwasiliana na wateja wetu, kuwashukuru kwa kuendelea kutuamini, na kuwadhihirishia jinsi tunavyothamini uaminifu wao,” alisema Annaroberta Mango, Mkuu wa Huduma kwa Wateja wa Bank of Africa -Tanzania.
Aliongeza Shughuli muhimu wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja na Mwezi wa 2025 ni pamoja na siku za kuwashirikisha wateja – vipindi shirikishi katika matawi ili kusikia moja kwa moja maoni kutoka kwa wateja, utambuzi wa wadau waliofanikisha mabadiliko chanya – Kutambua wateja bora, wafanyakazi, na wanajamii wanaowezesha ari ya huduma nzuri, na kutembelea jamii – shughuli za CSR ili kupanua huduma zaidi nje ya majengo ya benki kupitia timu za wafanyakazi wetu kwenye matawi.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi , Asupya Nalingigwa alifafanua kwamba wiki hii itakuwa pamoja na mambo mengine ni kutembelea wateja kwenye sehemu zao za biashara na kubadilishana nao mawazo na kujifunza pia kutoka kwao.
Mohammed Bargash Hamud akizungumza kwa niaba ya wateja alisema kwamba benki hiyo imekuwa ikitoa huduma nzuri za kifedha pamoja na mikopo ambayo kwa kiasi kikubwa imewasaidia wao kufanikiwa kibiashara.
“tumekuwa na benki kwa takribani miaka 30 katika huduma za kifedha tutaendelea kufanya nao kazi kwa minajili ya kukuza ushirikiano wetu nao kwenye huduma za kifedha hapa nchini,’ alisema
Bank of Africa -Tanzania inawaalika wateja, wadau, na wabia kujumuika katika kusherehekea tukio hili muhimu na kuendelea kutengeneza mustakabali ambapo ubora wa huduma za kibenki daima ni “Dhamira: Inawezekana”.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa- Tanzania, Wasia Mushi katika picha ya pamoja mteja wa benki hiyo, Mohamed Bargash Hamud na wafanyakazi wa kitengo cha huduma kwa wateja kwenye uzinduzi wa wiki ya wateja iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana