Benki ya DCB Commercial Bank Plc imezindua rasmi kampeni yake mpya iitwayo “Tuko Ground na Wenyewe”, yenye lengo la kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuhamasisha matumizi ya huduma za kidigitali nchini.
Kupitia kampeni hiyo, wateja wa DCB wataweza kufungua akaunti kwa njia ya mtandaoni wakiwa popote walipo na kutuma fedha bure kwenda benki nyingine au mitandao ya simu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Sabasaba Moshingi, Mkurugenzi wa Mikopo na Hatari za Kibenki, Deogratius Tadei, alisema kampeni hiyo imelenga kupunguza gharama za huduma za kifedha na kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiunga na mfumo rasmi wa kibenki.
“Tunataka kuona kila Mtanzania anapata huduma za kifedha bila vikwazo vya umbali au gharama. Hii kampeni ni sehemu ya jitihada zetu za kujenga benki jumuishi na ya kisasa,” amesema Tadei.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko, Huduma kwa Wateja na Huduma za Kidigitali wa DCB, Geophrey Magugi, amesema kampeni hiyo inalenga pia kuhamasisha jamii kutumia mifumo ya malipo isiyotumia fedha taslimu, jambo linaloendana na mkakati wa Serikali wa kujenga uchumi wa kidigitali.
“Tunataka huduma za DCB ziwe sehemu ya maisha ya kila siku ya Mtanzania kupitia teknolojia. Hii itarahisisha miamala, kuongeza ufanisi na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu,” amesema Magugi.
Katibu wa Mradi kutoka Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Johanes Msuya, amepongeza DCB kwa ubunifu huo akisema utasaidia kuongeza ushiriki wa wananchi katika huduma za kifedha rasmi.
Naye mteja wa benki hiyo, Salma Athman, amesema huduma hizo mpya zitasaidia kupunguza muda na gharama za kupata huduma za kifedha, hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya pembezoni.