*Ni maelfu ya wananchi Jiji la Mwanza wajitokeza kumpokea… “Mwanza ni nyumbani”
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mwanza
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameanza kampeni katika Mkoa wa Mwanza ambapo leo Oktoba 7,2025 amehutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo la Nyamagana.
Katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika eneo la Buhongwa mkoani Mwanza Dk.Samia amewaambia wananchi wa Mwanza kuwa huo ni mkoa muhimu kwa biashara, uzalishaji, kilimo na uvuvi huku akisisitiza kipeumbele cha Serikali ni katika huduma za jamii.
Dk. Samia amesema kwamba kazi ya CCM na Serikali ni kuendeleza na kukuza nguzo kuu za uchumi kwa mkoa huo lakini nguzo hizo zinatanguliwa na maendeleo ya jamii zikiwemo huduma za afya ya jamii, maji na nishati kwa ajili ya kurahisha shughuli za uzalishaji na usalama wa wananchi.
“Tumeweka nguvu kubwa kwenye maendeleo ya jamii na alafu maendeleo ya kiuchumi yanafuatia,” amesema na kuongeza katika miaka mitano iliyopita katika Wilaya ya Nyamagana Serikali imeboresha hospitali ya wilaya, imejenga vituo vinne vya afya, shule sita za sekondari na nane za msingi.
Pia, amesema Serikali imejenga mabweni mawili na uzio kwa ajili ya watoto wenye uhitaji maalum katika Shule ya Msingi Buhongwa.
Ameongeza vilevile Serikali imefanya uwekezaji katika sekta ya maji.”Nakumbuka ziara yangu ya kwanza nikiwa Rais pale Butimba nilisimama nilipokelewa na ndoo za kinamama wakaniambia sisi hatuna maji. Nikawaahidi nitajitahidi nilete maji.
“Nataka niseme kijana wenu ( Waziri wa Maji Jumaa Aweso) yupo hapa. Nilikuwa nikimkaba na kazi nzuri ameifanya. Tumetekeleza mradi mkubwa wa Butimba wa sh. bilioni 71.7.
“Mradi huo umewezesha kuwafikishia maji safi na salama wakazi 450,000 wa Buhongwa, Nyegezi, Igoma na maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo.Pia Serikali imetekeleza mradi mwingine wa sh. milioni 864 iliyonifaisha wakazi wa jiji hilo.
Akieleza zaidi amesema kuwa miradi mingine ya maji iliyotekelezwa kwa Sh.bilioni 46 ipo katika maeneo ya Buhongwa, Kishiri na maeneo mbalimbali ya mkoa huo ikiwa imefikia asilimia 85.
Amtoa ahadi ya kuikamilisha miradi hiyo na miradi ya upanuzi chanzo cha maji Kapripoint ili kuimarisha zaidi upatikanaji maji.
Kuhusu changamoto ya kukatika maji, amesema Serikali ilimtuma Katibu Mkuu Wizara ya Maji kushughulikia changamoto hiyo kazi ambayo imefanyika kwa ufanisi.
“Kuna tatizo la presha ya maji kuwa ndogo baadhi ya maeneo hasa yale ya miinuko ambapo serikali tunajenga matenki makubwa maeneo ya Nyamazobe lita milioni tano, Buhongwa lita milioni 10 na Fumagila ya juu tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10.
Amesema ujenzi wa matanki hayo umefikia asilimia 35 na kwamba kazi hiyo wataimaliza na baada ya kumaliza mtiririko wa maji utakuwa mzuri, yatapatikana saa 24.”
Kuhusu ujenzi miundombinu ya barabara amesema serikali imetekeleza ujenzi wa barabara ya Buhongwa -Igoma yenye kilometa 14 kwa sh. bilioni 22.7 ambapo ujenzi wake ulienda pamoja na madaraja ya Mbuyuni na Mabatini kwa Sh.bilioni 11.2 ujenzi ambao unaendelea.
Alieleza kuwa serikali iliahidi kujenga barabara ya Mwanza City Centre – Igoma – Kisesa.”Ili kuhakikisha ubora wa barabara Serikali itaongeza bajeti ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) waendelee na ujenzi wa barabara za ndani.
Pia, amesema kiwanja cha Ndege Mwanza serikali itakikamilisha kuwa cha kimataifa ili kianze kazi.
Mgombea urais Dk.Samia amesema pia kwa upande Nyamagana, Serikali imejenga miundombinu ya kituo cha mabasi Nyegezi na soko kuu la mjini kati.
“Ni miundombinu ya kisasa inayotoa ajira na kuongeza mapato kwa halmashauri. Lakini SGR inaendelea hiyo ndiyo CCM.
Amesisitiza kuna ujenzi wa masoko yaliyopangwa kujengwa na kuboreshwa kiwemo soko la mchafukuonga, soko la samaki Mkuyuni, Nyegezi na soko la mazao Igoma.
Ameongeza kuwa masoko mengine ni Mabatini, Buhongwa, Bukarika, Tambukareli na Butimba ambayo yatajengwa kwa kushirikiana na halmashauri.
Dk.Samia amesema kwamba ahadi ya CCM ni kuendelea kuiboresha Mwanza kuifanya kuwa jiji kweli kweli.
Katika hatua nyingine amesema asilimia 10 ya vikundi mbalimbali vimekuwa vikinufaika kupitia mikopo ya halmashuri ambapo bilioni tisa zimetolewa huku akitoa mwito kwa vikundi kurejesha mikopo ili wengine waweze kukopa.