Arusha. Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) limeridhia azimio la kulitaka Baraza la Mawaziri na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuharakisha mchakato wa kuwa na bima ya afya kwa wote, ili kuwa na jamii yenye watu wenye afya njema kwa lengo la kuongeza uzalishaji.
Akiwasilisha hoja hiyo leo Jumanne, Oktoba 7,2025 katika mkutano wa kwanza, mkutano wa nne wa Bunge la tano, mbunge wa Eala kutoka Rwanda, Balozi Fatuma Ndangiza amesema ili jumuiya isonge mbele Baraza la Mawaziri na nchi wanachama hawana budi kusukuma juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma sahihi za afya.
Balozi Ndangiza amesema nchi wanachama zilikubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusu afya za wananchi wao, pamoja na taasisi za zinazofanya tafiti za kiafya kushirikiana na kuoanisha sera za nchi hizo na kubadilishana uzoefu ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Napenda kushukuru Baraza la Mawaziri wa EAC kwa kuanzisha taasisi ya Utafiti wa Afya ya Jumuiya hii (EAHRC), iliyopo nchini Burundi kwa ajili ya kuratibu juhudi za kufanya tafiti, mikakati, mipango na sera zenye lengo la kuongeza usalama na ubora kwa wananchi kupata huduma bora za afya,” amesema Balozi Ndangiza.

Amesema nchi za Tanzania, Kenya na Rwanda zinafanya vizuri miongoni mwa nchi wanachama kwa idadi ya wananchi walioandikishwa kupata huduma ya matibabu kupitia huduma ya bima katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, licha ya nchi wanachama kushindwa kutenga asilimia 15 ya bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya sekta ya afya kulingana na makubaliano ya Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2001.
Amefafanua kuwa nchi wanachama zinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti katika kuwekeza kwenye sekta ya afya jambo ambalo ni kikwazo katika kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma ya bima ya afya kwa wote.
Wakichangia hoja hiyo, mbunge wa Eala kutoka Tanzania, Dk Gladness Salema amesema suala la huduma ya bima ya afya kwa wote linapaswa kuangaliwa kwa mapana yake na sio kuangalia kipengele kimoja pekee cha upatikanaji wa fedha, pia waangalie eneo la huduma zinazotolewa kwa wagonjwa.
“Tunapozungumza huduma ya bima ya afya kwa wote tunamaanisha ni mada ambayo hatuwezi kuipuka kwa sababu inahusu haki za binadamu, na nitumie nafasi hii kutambua juhudi ambazo zimeendelea kufanywa na Serikali zetu kuboresha mifumo ya afya tukitambua kuna maendeleo ambayo yamefikiwa.
“Huduma za bima ya afya kwa wote ni maono ambayo tunapaswa kuyafikia hapa nchini Tanzania tumepitisha sheria ambayo inalenga kufikia malengo ya huduma ya afya kwa wote.”
“Najua pia Rwanda na nchi zingine, lakini tunapozungumzia huduma ya afya kwa wote tunapaswa tuangalie maeneo yote yanayohusika na sio eneo moja la upatikanaji wa fedha bali pia huduma yenyewe inayotolewa na idadi ya watu wanaopata huduma,” amesema Dk Gladness.
Wengine waliochangia ni mbunge kutoka Kenya, Kanini Kega amesema changamoto ya wananchi kupata huduma ya bima ya afya kwa wote ni kutokana na idadi kubwa kutokua kwenye ajira rasmi, hivyo mfumo kushindwa kuwapata na kuomba utaratibu uwekwe ili kila mwana Afrika Mashariki anufaike na huduma za afya kwa wote.
Akizungumza kwa niaba ya baraza la mawaziri wenzake, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa Uganda, James Magode amesema hoja hiyo imekuja wakati muafaka na inafaa kutekelezwa kwa haraka kwa manufaa ya jumuiya.