FIFA yawapa ulaji Karia, Hersi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), limewapa nafasi mpya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Rais wa Klabu ya Yanga, injinia Hersi Said.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom, kwenda kwa viongozi hao imesema Karia ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kamati ya Soka la Ufukweni.

Rais wa Soka Haiti, Thierry Ariontima ndiye anayeongoza kamati hiyo ambapo Karia anakuwa Mwafrika wa nne kuingia kwenye kamati hiyo, sambamba na Fesal Sidat (Msumbiji), Samir Sobha (Mauritius) na mmoja kutoka Shelisheli.

Mbali na nafasi hiyo, Karia pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lakini pia Mjumbe wa Kamati ya Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

Wakati Karia akipata nafasi hiyo, Hersi amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano yote ya wanaume ya klabu Duniani kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2025 hadi 2029.

Hersi ni kama anaendelea kujitanua zaidi kwenye soka duniani ambapo nafasi hiyo inakuja wakati ambao akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu Afrika (ACA).

Uteuzi wa viongozi hao umetangazwa Oktoba 6, 2025 kwenye Mkutano Mkuu wa CAF, uliofanyika jijini Kinshasa nchini DR Congo kisha wahusika kuandikiwa barua rasmi Oktoba 7, 2025.

Naye Neema Haji ambaye ni mratibu wa timu za Taifa Wanawake Tanzania, ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Soka la Vijana Wanawake Duniani.