United People’s Democratic Party (UPDP), ni chama kilichopata usajili wa kudumu Februari 4, 1993.
Kikokotoo cha kalenda kinatupa majibu kwamba, UPDP ni chama chenye umri wa miaka 32 na miezi nane iliyotimia.
Ni chama ambacho kimekuwepo kwenye kila uchaguzi, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, Julai mosi, 1992.
Tanzania ipo kwenye msimu wa uchaguzi, kwa ajili ya kupata viongozi wataoiongoza nchi muhula ujao wa miaka mitano. Ndani ya visiwa vya Zanzibar, katika uchaguzi mkuu 2025, matumaini yote ya UPDP yapo kwa mpeperusha bendera wao, Hamad Mohamed Ibrahim ambaye ni Katibu Mkuu wa UPDP Taifa.
Anasema kuwa, chama chake kinamfahamu kuwa amekomaa kisiasa, ndiyo maana kimempa tiketi ya kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Ibrahim anajinasibu kwamba, Wazanzibari watakuwa na Rais bora, endapo watamwamini na kumpigia kura kwa wingi.
Kuhusu nafasi yake ya kushinda, Ibrahim anawatoa hofu Wazanzibari kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki.
Yeye binafsi, kwa nafasi yake ya mgombea urais, ataweka mawakala kila kituo cha kupigia kura, vilevile wagombea ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani, wenye tiketi ya UPDP, watakuwa na mawakala. Ibrahim anawahakikishia wapigakura kwamba hakuna haki itadhulumiwa.
Julai mosi, 1964, kwenye Kata ya Kangagani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini, Pemba, familia ya baba, Mohamed Ibrahim Kombo na mama, Bikombo Sharif Shoka, ilipata mtoto wa kiume, wakampa jina la Hamad. Ni mtoto wa nne miongoni mwa watoto saba wa familia hiyo.
Hamad, ndiye Hamad Mohamed Ibrahim, unapotaja jina lake kwa ukamilifu.
Mwaka 1972, Ibrahim alianza darasa la kwanza, Shule ya Msingi Kangagani.
Katika shule hiyo, Ibrahim alisoma darasa la kwanza mpaka la tatu. Mwaka 1975, wazazi wa Ibrahim walihamia Unguja, hivyo aliendelea na darasa la nne Shule ya Msingi Rahaleo, iliyokuwepo Kariakoo, Zanzibar.
Shule ya Rahaleo ilibadilishwa jina. Kwa sasa eneo la iliyokuwa Shule ya Rahaleo, kuna shule tatu ambazo ni Shule ya Msingi Mwembeladu, Shule ya Msingi Mwembeshauri na Shule ya Sekondari ya Dk Ali Mohamed Shein.
Ibrahim alimaliza elimu ya msingi Rahaleo, kisha alijiunga na Shule ya Sekondari Kangagani, kuanzia mwaka 1978. Mwaka 1980, alifanya mtihani na kufaulu kuendelea na kidato cha nne, ambacho alisoma Shule ya Sekondari Utaani, iliyopo wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini, Pemba. Alihitimu elimu sekondari mwaka 1981.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne hayakuwa mazuri kwa Ibrahim. Mwaka 1983, Ibrahim alijiunga na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Zanzibar.
Alipata mafunzo ya kijeshi kwa mwaka mmoja, baada ya hapo aliingia mtaani kufanya shughuli ndogondogo, akitafuta mtaji wa biashara.
Mwaka 1990, Ibrahim alianza biashara za kutoka Zanzibar na kuzunguka nchi mbalimbali. Mathalan, alikuwa akisafirisha viatu na vinyago kwenda Burundi, halafu alinunua vitenge Burundi na kuviuza Dar es Salaam.
Alikwenda Kenya kununua khanga na kuziua Zanzibar. Alifanya biashara ya bidhaa za baharini kati ya Msumbiji na Mombasa, Kenya.
Mwaka 1983, Ibrahim alipojiunga na JKU, kulikuwa na wito wa kujisajili na kupewa kadi ya CCM kwa hiyari.
Ibrahim alisajiliwa rasmi kama mwanachama wa CCM mwaka 1983. Uanachama wake ulidumu kwa miaka 17. Mwaka 2000, Ibrahim alijiunga na UPDP, chama ambacho amedumu nacho hadi sasa.
Ndani ya UPDP, Ibrahim alianzia chini kabisa. Kwanza kama mwanachama wa kawaida, akawa anafanya kazi ndogondogo kwenye Ofisi Kuu ya UPDP, ambayo wakati huo ilikuwa Mji Mkongwe, Zanzibar. Kwa sasa, Ofisi Kuu ya UPDP Zanzibar ipo Mtoni Kidatu, Garagara, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Mwaka 2005, Ibrahim aligombea ubunge Jimbo Mfenesini, lililopo Wilaya ya Magharibi A. Hakushinda. Alitoka wa tatu, nyuma ya mgombea wa CCM aliyeshinda na wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyetoka wa pili.
Uchaguzi mkuu wa 2010, UPDP, ilimteua Ibrahim kuwa mgombea mwenza wa urais, akishirikiana na aliyekuwa mgombea urais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fahmi Nassor Dovutwa.
Kipindi hicho, Dovutwa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa UPDP Taifa.
Mwaka 2013, Dovutwa, akiwa Mwenyekiti wa UPDP, alimpendekeza Ibrahim kuwa Katibu Mkuu wa UPDP, kisha Halmashauri Kuu ya chama hicho ilimthibitisha, katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Rombo Greenview, iliyopo Barabara ya Shekilango, Ubungo, Dar es Salaam.
Uchaguzi Mkuu Tanzania 2015, Ibrahim akiwa Katibu Mkuu wa UPDP, aliteuliwa kwa mara nyingine kuwa mgombea mwenza wa urais chama hicho. Mgombea urais alikuwa Dovutwa.
Ulipofika uchaguzi mkuu wa 2020, UPDP walimpa Ibrahim tiketi ya kuwa mgombea urais wa Zanzibar.
Kwa mantiki hiyo, Ibrahim anawania urais Zanzibar kwa mara ya pili.
Na anapoitupa karata yake kipindi hiki cha kampeni, Ibrahim anasema anataka awe Rais wa Zanzibar ili amalize tatizo la umeme kwa asilimia 100 na ikiwezekana Zanzibar ndiyo iuze nishati hiyo nje ya nchi.
Ibrahim anasema kuwa, Zanzibar kwa sasa inategemea umeme kutoka Tanzania Bara, ambao hautoshelezi mahitaji ya nishati hiyo visiwani humo.
Anaongeza kwamba, umeme huo kutoka Tanzania Bara gharama yake ni kubwa.
Ibrahim anasema akiwa Rais, ataanzisha mara moja mchakato wa kusimika vinu viwili vya nyuklia, kimoja kitakuwa Pemba, kingine Unguja.
Vinu hivyo vya nyuklia vitakuwa na kazi moja tu; kufua umeme.
Anaeleza kuwa, umeme utokanao na nyuklia, utakuwa mwingi, utatosheleza Zanzibar yote na ziada.
Ibrahim anasema kuwa, umeme wa ziada utauzwa nje ya nchi ili kuwa moja ya vyanzo vya mapato kwenye Serikali atakayoiongoza.
“Nikiwa Rais wa Zanzibar, kwa gharama yoyote lazima tusimike vinu vya nyuklia vya kufua umeme.”
Mpango mwingine wa Ibrahim ni kuifanya Zanzibar kuwa ya viwanda.
Anasema karafuu ni zao kubwa la kibiashara, lakini bado halijainufaisha Zanzibar inavyotakiwa.
Ibrahim anaeleza, kwamba ataanzisha viwanda kwa ajili ya kuchakata karafuu ili itoe bidhaa kama sabuni, mafuta, dawa na kadhalika.
Uwepo wa viwanda, kwa mujibu wa Ibrahim, utawezesha vijana kupata ajira. Thamani ya karafuu itapanda, hivyo kuwanufaisha zaidi wakulima.
Anaahidi akiwa Rais, asilimia 20 tu ya karafuu inayolimwa Zanzibar ndiyo itauzwa nje, lakini asilimia 80, itabaki Zanzibar, ichakatwe na kuzalisha bidhaa badala ya kuuza malighafi.
Vijana wenye umri wa kuoa, urais wa Ibrahim utakuwa neema kwao.
Anasema, kijana wa kiume atakayetaka kuoa, kila mmoja, atapewa Sh2,000,000 ya mahari. Pia, mwanamke atakayechumbiwa, naye atapewa Sh2,000,000 ili imsaidie kuanzisha biashara baada ya kufunga ndoa.
maana hiyo, kila ndoa, itapokea ruzuku ya Sh4,000,000.
Sekta ya afya, Ibrahim anasema Zanzibar ina miundombinu ya kutosha ya kutolea huduma za afya, changamoto ni vifaa tiba na dawa.
Anaahidi kuweka mkazo katika vifaa tiba, dawa na madaktari bingwa ili Wazanzibari wapate huduma bora za afya.
Anasema, Zanzibar kwa sasa huduma za afya zinatolewa bure. Hilo analipongeza kwa moyo mkunjufu. Ibrahim anasema kuwa akiwa Rais, huduma za afya zitaendelea kuwa bure Zanzibar, lakini ataongeza ufanisi wa huduma. Anaahidi kwamba Zanzibar chini ya Serikali ya UPDP, watu watatoka maeneo mbalimbali duniani na kuingia Zanzibar kutibiwa.
Haitakuwa kama sasa, Wazanzibari ndiyo wanakimbilia nje kutibiwa.
Ibrahim anasema atakuwa na mbinu bora za ukusanyaji wa mapato. Ataufanyia kazi Uchumi wa Bluu, uweze kutoa matokeo bora kwa Wazanzibari.
Muhimu zaidi, Ibrahim anaahidi kushughulikia mfumo wa elimu, ili wahitimu wa Kizanzibari wawe na umahiri wa kusimamia miradi na shughuli za kiuchumi ndani ya visiwa hivyo.
“Shule na vyuo Zanzibar, vitatoa wanafunzi wenye utaalamu wa hali ya juu. Serikali itawezesha vijana wa Kizanzibari kupelekwa nje kuongeza utaalamu ili wakirejea waweze kusimamia shughuli za kiuchumi Zanzibar,” anasema Ibrahim na kuongeza: “Serikali inatumia fedha nyingi kuwalipa wageni, Serikali ya UPDP chini ya uongozi wake, itahakikisha wenyeji ndiyo wanaongoza njia zote za kiuchumi Zanzibar.”
Halima Said Abdallah ni mke wa kwanza wa Ibrahim. Anaye mke wa pili, Aziza Amour Suleiman. Ibrahim ni baba wa watoto saba, wanne kutoka kwa Halima na watatu aliowapata na Aziza.
Ibrahim anawataka wananchi wawe makini, wachague viongozi ambao wataweza kuipa nchi maendeleo. Viongozi ambao wataweza kutunza amani ya nchi kwa sababu wanatambua amani na utulivu ni tunu ya taifa.