KIPA wa JKT Tanzania, Ramadhan Chalamanda amesema anafurahia nafasi anayopata katika kikosi hicho alichojiunga nacho msimu huu akitokea Kagera Sugar, huku akifichua kinachombeba akimtaja kocha Ahmad Ally.
Chalamanda aliyeanzishwa mechi zote tatu zilizopita katika Ligi Kuu Bara, alisema kupata nafasi ya kucheza kunatokana na kubebwa na mbinu Ahmad na jopo zima la benchi la ufundi ya timu.
Kipa huyo aliyeshuka daraja na Kagera msimu uliopita kabla ya kuibukia JKT Tanzania, ameiambia Mwanaspoti kuanza katika mechi zote aliizocheza haimfanyi kujiona bora kuliko wenzake aliowakuta kikosini.
Amesema hawezi kupima kiwango bora bila kumtaja kocha ambaye ameendelea kumnoa kuanzia mazoezini ili kuhakikisha anazidi kuwa imara.

“Maisha ya kupata namba ndani ya JKT yalianzia mazoezini ambako kocha ndipo ananipa maelekezo ya jinsi ya kuwa kipa nitakayeweza kutetea timu mbele ya wapinzani. Nilipoanza kazi kocha alipata muda wa kukaa na mimi na kuniambia natakiwa kupambana na taratibu naendelea kuingia kwenye mfumo wake, hivyo ni suala la muda tu nitaimarika zaidi ya hapa,” amesema.

JKT Tanzania imecheza mechi tatu ikiwa haijapoteza, huku ikitoka sare ya 1-1 na Mashujaa na Azam ilhali ikishinda 2-0 dhidi ya Coastal Union.