Dar es Salaam. Kusimamia kikamilifu ajenda ya nishati safi ya kupikia ya Watanzania wanne kati ya watano kufikia mwaka 2034, kutafuta rasilimali zaidi, nishati jadidifu, ni miongoni mwa ajenda itakazozisimamia Tanzania katika mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30).
Mkutano huo utakaofanyika jijini Belem nchini Brazil Novemba 10 hadi 21, 2025 utawakilishwa na ujumbe wa Tanzania pia unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 2024 mkutano huo ulifanyika jijini Baku, Azerbaijan na uliwakilishwa na Makamu wa Rais.
Mengine ni suala la fedha, kujengeana uwezo katika taasisi za serikali na kiraia, teknolojia mpya ambazo zitakuja kusaidia kukabiliana na mabadiliko hususani katika kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kupunguza gesijoto.
Vilevile biashara ya kaboni, mabadiliko na ustahimilivu, hasara na uharibifu, kuhakikisha mfuko wa hasara na uharibifu unaanza kufanya kazi na nchi zilizo hatarini kama Tanzania zinapata fursa ya kuutumia.
Pia, fedha za hali ya hewa, uchumi wa buluu, usimamizi endelevu wa misitu, ushiriki jumuishi, kuhakikisha sauti za wanawake, vijana, watoto, na jamii za wenyeji zinasikika katika kuunda suluhisho za hali ya hewa.
Katika mkutano huo Tanzania inatarajia kubeba vipaumbele vya kitaifa na bara la Afrika katika suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, kwa Tanzania, huu si mkutano wa mazungumzo bali unahusu kuanzisha ubia na kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali ya kutosheleza kwa ajili ya kulinda watu, mifumo ikolojia na uchumi stahimilivu kutokana na athari zinazoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza leo Dar es Salaam Jumanne Oktoba 7, 2025 kwenye kikao cha maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda Brazil, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia mazingira, Peter Msoffe amesema ushiriki wa Tanzania ni malengo na mkakati katika suala zima la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Bahati nzuri maazimio yote ya mkutano uliopita yameshafanyiwa kazi kwa asilimia kubwa. Ahadi tulizopata za kusaidia masuala ya mazingira kwa Tanzania zaidi ya asilimia 80 ya ahadi zimetekelezwa ikiwemo fedha na miradi iliyoahidiiwa,” amesema.
Balozi, Noel Kaganda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amesema ni jukumu la pamoja katika kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko hayo suala linaloenda sambamba na dira ya 2050.
“Mkutano huu unabeba ajenda kubwa ya nchi katika kuhimiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano mbalimnbali ikiwemo kuongeza fedha, teknolojia, uhifadhi wa misitu hivyo ni fursa kwa nchi yetu kushiriki,” amesema.
Amesema Tanzania inazalisha hewa ukaa kwa kiwango kidogo sana na inauwezo wa kutumia misitu yake kumeza kaboni yenye athari.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) nchini Tanzania Clara Makenya ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kukutana na kupata uelewa wa pamoja kuelekea COP 30 mkutano unaojumuisha wadau mbalimbali wa Mazingira kutoka maeneo tofauti tofauti.
“Wito wangu kuna mijadala mbalimbali na kila mdau ana jukumu muhimu la kujiandaa kama ni upande wa uchumi wa Buluu, Nishati au eneo lingine ajue eneo lipi anaenda nalo kwa ajili ya kujipanga kimkakati na wadau wa dunia nzima na pia kujua kitu gani anaenda kutoa na kujua mdau yupi anaenda kusapoti agenda anayoiwasilisha na kufaha mu kuwa wanaeda kama nchi na kuweza kupata matokeo ambayo yanatarajiwa,” amesema.
Awali katika ufunguzi wa kikao cha jana Jumatatu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema Tanzania kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kundi la Nchi za Afrika la Watalaamu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Africa Group of Negotiators – AGN) hivyo, inatarajiwa kuongeza majadiliano na kuzingumza kwa niaba ya bara la Afrika katika mijadala inayohusu mabadiliko ya tabianchi itakayofanyika wakati wa COP30.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa CAN Tanzania Dk Sixbert Mwanga amesema kuwepo kwa kikao hicho kitasaidia kuwaandaa wadau wote kuwa na kauli moja na kuifanya Tanzania kupata kile kilichokusudia katika COP30.
Hata hivyo, mkutano huo wa 30 unatarajiwa kufafanua hatua za haraka katika kukusanya fedha kiasi cha Dola za Marekani 1.3 Bilioni zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.