Wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu taarifa za kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, Jeshi la Polisi linamtafuta ndugu aitwaye Augustino Polepole aliyejitambulisha kama kaka.
Kwa mujibu wa ndugu huyo, Polepole ametekwa usiku wa kuamkia jana nyumbani kwake na tayari Polisi limeeleza kuwa, linaendelea na uchunguzi baada ya kupata taarifa hizo.
Hata hivyo, wakati bado kukiwa na sintofahamu kuhusu waliomteka na mahali alipo, Polisi wamesema wanamtafuta Augustino ili atoe ushirikiano kwa chombo hicho kubaini ukweli wa madai hayo.
Awali, Jeshi la Polisi Tanzania jana Kotoba 6, 2025 kupitia taarifa yake lilieleza kuwa tayari uchunguzi wa kina kufuatia madai hayo ya Augustino, yameanza kufanyiwa kazi.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Jumanne, Oktoba 7, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, imesema kuwa uchunguzi huo ulianza baada ya kusambaa kwa taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii.
“Jeshi la Polisi lilifungua jalada la uchunguzi tangu Oktoba 6, 2025 na tayari limeanza kukusanya ushahidi na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ili kubaini ukweli wa madai hayo.
“Kwa sasa tunaendelea kumtafuta Augustino Polepole ili apatiwe nafasi ya kutoa ushirikiano na kutoa maelezo ya kina na vielelezo vinavyoweza kusaidia kufafanua madai yake, ikiwemo hoja kuwa ofisa wa polisi alihusika katika tukio hilo,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa uchunguzi unalenga pia kubaini kama Polepole alikuwa akiishi au alikuwa mpangaji katika nyumba inayodaiwa kuwa eneo la tukio.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina na litaendelea kuwajulisha wananchi matokeo ya awali mara tu hatua muhimu zitakapokamilika,” imehitimisha taarifa hiyo.
Mwananchi limefika kwenye nyumba anayodaiwa alikuwa akiishi ilipo Boko Basihaya jijini Dar es Salaam na kujionea hali ilivyo ikiwemo uharibifu uliofanyika kwenye nyumba hiyo.
Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia mitandao yetu.