Dar es Salaam. Mwanasayansi maarufu duniani katika tafiti za tabia za wanyama, Jane Goodall (91), aliyefariki dunia akiwa nchini Marekani na kusababisha simanzi duniani kote, hususan Tanzania ambako alifanya tafiti zake kwa muda mrefu.
Msiba wake upo nyumbani kwake Mikocheni, jirani na nyumba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambapo viongozi na wananchi mbalimbali wanaendelea kusaini kitabu cha maombolezo.
Getrude Mongela, mwanadiplomasia na kiongozi wa zamani, amemuelezea Goodall kama mwanamke wa kipekee aliyetoa mchango mkubwa katika kulinda wanyamapori na mazingira.
“Nilianza kumfahamu kabla sijamuona. Wakati huo nilikuwa mwalimu wa historia. Tulipojuana kwa karibu zaidi, ilikuwa baada ya kifo cha mumewe, Brayson mmoja wa mawaziri wa kwanza wa Tanzania baada ya uhuru. Nilimsubiri uwanja wa ndege aliporejea na majivu ya marehemu ili kuyatawanya katika Bahari ya Hindi, kama alivyoelekezwa na mumewe,” amesema Mongela leo Jumanne Oktoba 7, 2025 alipozungumza na Mwananchi nyumbani kwa marehemu.
Amesema urafiki wao uliendelea na baadaye Goodall alimualika kujiunga na bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Jane Goodall Institute, yenye matawi duniani kote yenye chimbuko lake Tanzania katika Hifadhi ya Gombe mkoani Kigoma.
“Jane alileta umaarufu mkubwa kwa Tanzania, kwa sababu tafiti zake zilivutia watalii wengi kuja Gombe kuangalia sokwe mtu. Alikuwa mpenzi wa wanyama, mwenye moyo wa huruma na aliyepinga kwa nguvu zote vitendo vilivyohatarisha makazi ya sokwe,” amesimulia Mongela.
Naye James Lembeli, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jane Goodall, amesema Goodall alikuwa mtu wa kipekee aliyependa kila kiumbe hai.
“Alipenda watu, alijali wanyama na alihangaika kuhakikisha dunia inabaki salama kwa wote. Nilipomfahamu kwa karibu zaidi ilikuwa kipindi Serikali ilipopanga kujenga barabara ya lami Serengeti. Nilijiunga na kampeni za kimataifa zilizopinga hatua hiyo na Jane alikuwa mstari wa mbele. Tangu hapo akanilea katika misingi ya upendo, haki na ulinzi wa mazingira,” amesema Lembeli.
Amesema Goodall alibadilisha mtazamo wa jamii kuhusu sokwe, akionesha kuwa hawana tofauti kubwa na binadamu.
“Nimezunguka naye maeneo mengi duniani kuhamasisha ulinzi wa mazingira. Alikuwa mfano wa pekee,” amesema Lembeli.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Jane Goodall nchini, Fredrick Kimaro, maandalizi ya mazishi yanaendelea kwa kushirikiana na familia ya marehemu iliyopo Uingereza.
“Kwa sasa mwili wake bado upo California, Marekani. Unatarajiwa kusafirishwa kwenda Uingereza kwa maziko ambako ana makazi pia. Hapa Dar es Salaam viongozi na wananchi wanaendelea kusaini kitabu cha maombolezo,” amesema Kimaro.
Akimuelezea Goodall, Kimaro amesema, “Tangu mwaka 1960, enzi za Tanganyika, tafiti zake zilileta mageuzi makubwa. Alikwenda porini kufanya utafiti kipindi ambacho dunia iliamini sayansi ni ya wanaume pekee. Mama yake ndiye aliyempa nguvu kuanza safari hiyo. Utafiti wake ulithibitisha sokwe wanaweza kutengeneza zana na wana hisia kama binadamu.”
Safari ya Goodall ilianza mwaka 1960 katika Hifadhi ya Sokwe ya Gombe Stream, Kigoma kwa mwaliko wa Dk Louis Leakey.

Akiwa na miaka 26 pekee na bila elimu rasmi ya chuo kikuu, alianzisha utafiti uliobadilisha historia ya sayansi duniani.
Kwa zaidi ya miaka 50 alijulikana kwa utafiti wa kina kuhusu sokwe mtu na tabia zao zinazofanana kwa karibu na binadamu, jambo lililovunja dhana za kijinsia na kisayansi.
Jane Goodall ameacha urithi mkubwa unaoendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tafiti za sokwe na uhamasishaji wa ulinzi wa mazingira duniani.