Lissu akubali yaishe pingamizi la Jamhuri

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imekataa ombi la Tundu Lissu, aliyeomba kupokewa maelezo ya maandishi ya shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Mahakama imekataa ombi la Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya kuwekewa pingamizi na waendesha mashtaka katika kesi hiyo.

Baada ya pingamizi kuwekwa, Lissu amekubaliana nalo kuwa amekosea utaratibu wa kisheria katika kuomba maelezo hayo yapokewe kama kielelezo.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno anayodaiwa kutamka kuhusu kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam.

Maneno yaliyoko kwenye hati ya mashtaka yanayodaiwa kutengeneza kosa la uhaini yanasomeka:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo) na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, imeendelea leo Oktoba 7, 2025 kwa ushahidi wa upande wa Jamhuri.


Lissu amemhoji maswali ya dodoso shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), George Bagyemu, ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu Dar es Salaam (DZCO).

Mshtakiwa ambaye anajitetea mwenyewe, amehoji maswali ya dodoso kuhusu ushahidi alioutoa Bagyemu jana Oktoba 6, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga.

Lissu amemuhoji shahidi iwapo aliandika maelezo yake kuhusu kesi hiyo mara mbili kwa nyakati tofauti? Shahidi amekubali kufanya hivyo.

Kwa kukubali huko, Lissu amemuonyesha nakala mojawapo ya maelezo hayo, shahidi akakubali ni yake.

Kisha akamuhoji iwapo anakubali kuyatoa mahakamani yapokewe na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa utetezi (wa Lissu). Shahidi akakubali, hivyo mshtakiwa akaiomba mahakama iyapokee.

Jamhuri ikapinga ombi hilo, ikiiomba mahakama isiyapokee ikidai mshtakiwa hakufuata utaratibu wa kisheria katika kuwasilisha maelezo ya shahidi kwa kusudi la kuyatumia kuhoji kuaminika kwake.

Wakili wa Serikali Mkuu, Ignas Mwinuka, amesema mshtakiwa hajatimiza matakwa ya kisheria ya namna ya kuhoji kuaminika kwa shahidi kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Rufani katika kesi mbalimbali.

Amedai kifungu cha 163 kikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 173 cha Sheria ya Ushahidi ya Tanzania (TEA) vinaeleza taratibu za kuzingatiwa katika kuhoji kuaminika kwa shahidi, huku akirejea mashauri kadhaa, likiwamo la rufaa namba 151/2018 ya Lilian Fotes dhidi ya Jamhuri iliyoamuliwa na Mahakama ya Rufani Septemba 20, 2022.

“Hapa mahakamani mshtakiwa ameanza hatua ya tatu kati ya hizo mahakama ilizoelekeza, kwa hiyo utaratibu haujazingatiwa,” amedai Mwinuka.

Vilevile, amedai Mahakama Kuu ilijadili mashauri ya Mahakama ya Rufani katika shauri la Jamhuri dhidi ya Mnawale Nyanda na wenzake tisa katika kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2022, iliyoamuliwa Oktoba 27, 2023.

Amesema katika uamuzi huo, mahakama ilieleza taratibu nane zinazopaswa kuzingatiwa katika kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika mashauri tajwa.

Miongoni mwa taratibu au hatua hizo ni kuwasilisha maombi chini ya kifungu namba 164, uthibitisho unaoweza kufanywa kwa kumuonyesha shahidi maelezo hayo na kumuongoza shahidi kusoma sehemu ya maelezo inayokusudiwa kuhojiwa.

“Kwa kuangalia maelekezo ya CAT na uamuzi wa Mahakama Kuu na vifungu tulivyovirejea, mshtakiwa hajazingatia taratibu hizo,” amedai.

Kwa upande wake, wakili Katuga amedai ni msimamo wa sheria kwamba, kielelezo kabla ya kupokewa mahakamani lazima kiwe kimethibitishwa na kipitie vigezo vya kisheria.

Amedai msimamo huo umetolewa na Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa rufaa ya Robson Mwanjilisi na wenzake watatu dhidi ya Jamhuri, rufaa mamba 154/1994.

Amedai msimamo wa Mahakama ya Rufani na utaratibu ulioainishwa na mahakama hiyo katika uamuzi kwenye mashauri mbalimbali waliyoyataja umetokana na kifungu cha 163(1) (3).

Katuga amesema ni jukumu la mwenye nia ya kupima kuaminika kwa shahidi kufuata taratibu hizo.

“Kwa hiyo mshtakiwa amerukia tu hatua ya tatu, ndiyo maana tunasema hakufuata utaratibu bila kujali shahidi wetu amesema hana tatizo, lakini ninyi waheshimiwa majaji lazima mfuate sheria,” amesema.


Amesema katika mazingira hayo, mshtakiwa hawezi kurudi nyuma kuanza upya, kwani sheria inamzuia kwa mujibu wa kifungu cha 131 cha TEA.

Kutokana na maelezo hayo, amedai mshtakiwa ameasilisha ombi hilo kabla ya muda, hivyo halina msingi na mahakama inapaswa kulitupa.

“Hivyo naunga mkono kuwa   yasipokewe,” amehitimisha Katuga.

Akijibu hoja za pingamizi, Lissu amesema anakubaliana na pingamizi la Jamhuri.

“Kama msimamo wa sheria ndivyo ilivyo, ninakubali kuwa nimekosea kuanzia hatua ya tatu, hivyo kuliko tupoteze muda ninakubali na niko tayari kuanza upya kama Mahakama ya Rufani ilivyoelekeza,” amesema.

Hata hivyo, Katuga amedai hawezi kurekebisha makosa kwa sababu ya kizuizi cha kisheria kurekebisha makosa/msimamo chini ya kifungu cha 131 TEA, Marejeo ya Mwaka 2023. Amedai hakitumiki katika mazingira hayo.

“Mimi nimeomba shahidi awasilishe nyaraka nikiamini kwamba, utaratibu wangu ni sahihi. Mawakili wa Serikali wamenikatalia kuwa utaratibu wangu si sahihi na mimi nimewakubalia kwa hiyo kizuizi cha kisheria kurekebisha makosa haihusiki hapa,” amesema Lissu na kuhitimisha:

“Bila kupoteza muda nimesema nakubaliana na pingamizi lao kuhusu utaratibu wa namna ya kuwasilisha nyaraka za namna hii, hivyo niko tayari kurudi nyuma kuanza upya kama walivyosema na kama nilivyouona utaratibu kwenye hizi nyaraka (nakala za kesi rejea) wala haina shida.”

Wakili Katuga amepinga hoja ya Lissu kurekebisha utaratibu akisisitiza sheria hairuhusu, akidai chini ya kifungu cha 131 cha TEA mtu akikosea hawezi kuja kurekebisha makosa hayo.

“Hii ni mahakama ya utaratibu si ya kujifunza/majaribio, mahakama ikiruhusu kurekebisha makosa mtu akiwa amekosea akiruhusiwa kurekebisha mwenendo hautaisha maana kila anayekosea atakuwa anakuja kuiomba kurekebisha,” amesema Katuga.

Amesisitiza kifungu cha 131 TEA kinazuia iwe na upande wa utetezi au Jamhuri kufanya marekebisho ya makosa ili kulinda mwenendo wa mahakama.

Akitoa uamuzi Jaji Ndunguru amesema baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kwa kuwa upande mmoja umekiri kukosea, jambo linalobishaniwa ni kuruhusiwa au kutokuruhusiwa kufanya marekebisho.


Jaji Ndunguru amesema pale upande mmoja unapokubali pingamizi, kuruhusu kufanya marekebisho ni kukinzana na utaratibu ambao ulishawekwa na Mahakama ya Rufani.

“Kwa hiyo, mahakama inakubaliana na pingamizi hili, hivyo inaikataa nyaraka hii,” amesema Jaji Ndunguru.

Baada ya uamuzi huo, Lissu ameendelea na maswali ya dodoso kwa shahidi huyo.