Mahakama Kuu Yaamua Hatima ya Mpina Oktoba 10 – Global Publishers



Mwanachama wa chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina, amesema kuwa matamanio yake makuu ni kuona anaruhusiwa kugombea nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisisitiza kuwa anataka kuonyesha utofauti wa kampeni na uongozi unaozingatia maslahi ya wananchi.

Mpina alitoa kauli hiyo Oktoba 6, 2025, nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala Kuu Dodoma), muda mfupi baada ya kusikilizwa kwa Shauri la Kikatiba Na. 24027 la mwaka 2025, analopinga kuondolewa kwake kwenye orodha ya wagombea urais dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Matamanio yangu makubwa ni kuona ninaruhusiwa kugombea ili kuonesha utofauti wa kampeni za kisiasa na namna ya kuongoza taifa letu. Nchi inahitaji viongozi wa aina mpya — wenye dira, uthubutu na uwazi,” alisema Mpina akiwa nje ya mahakama.

Mahakama hiyo, chini ya jopo la majaji watatu Jaji Frederick Manyanda, Jaji Sylvester Kainda, na Jaji Abdallah Gonzi  imetangaza kuwa itatoa hukumu ya shauri hilo Oktoba 10, 2025, saa 8:00 mchana.

Katika hatua ya leo, mahakama ilijiridhisha na utekelezaji wa amri ya kuwasilisha hoja kwa maandishi kutoka kwa pande zote mbili kabla ya kutangaza tarehe ya hukumu.

Kesi hiyo imeendelea kuvutia hisia na mjadala wa kisiasa, hasa kwa kuwa inahusisha hoja nyeti kuhusu haki za kugombea nafasi za juu za kisiasa na tafsiri ya Katiba kuhusu masharti ya wagombea urais nchini.