Dar es Salaam. Tundu Lissu, mshtakiwa katika kesi ya uhaini amechuana kwa maswali na shahidi wa kwanza wa Jamhuri, mchuano uliodumu kwa takribani saa sita.
Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno anayodaiwa kutamka kuhusu kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam.
Maneno yaliyoko kwenye hati ya mashtaka yanayodaiwa kutengeneza kosa la uhaini yanasomeka: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo, inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo), na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, imeendelea leo, Oktoba 7, 2025, kwa ushahidi wa upande wa Jamhuri.
Lissu amemhoji maswali ya dodoso shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Bagyemu, ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu Dar es Salaam (DZCO).
Mshtakiwa, ambaye anajitetea mwenyewe, amehoji shahidi maswali hayo kuhusu ushahidi alioutoa jana, Oktoba 6, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga.
Sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:
Lissu: Waeleze majaji, kama maudhui yenye uchochezi kwa umma ni kosa la uhaini au siyo kosa la uhaini?
Shahidi: Ni kosa la uhaini.
Lissu: Twende kwenye sheria kwanza. Shahidi, jana ulisema kosa la uhaini lipo katika kifungu 39(2)(e) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu?
Lissu: Nikupe usome hicho kifungu?
Lissu: Naomba nikusomee maneno ambayo nimeshtakiwa nayo (anasoma shtaka lake lote). Leo nipo gerezani siku 182, je, maneno haya yapo kwenye hati ya mashtaka?
Shahidi: Hayo uliyoyasoma hayapo, ila yapo kwenye maelezo yangu ya onyo.
Lissu: Kwenye haya niliyosoma, yapo kwenye hati ya mashtaka, kuna sehemu yoyote nimetaja neno la Serikali?
Shahidi: Ndiyo, ukisoma mpaka mwisho utaona.
Lissu: Neno Serikali lipo kwenye hiyo hati ya mashtaka?
Shahidi: Sijui unatafsiri vipi? Lipo.
Lissu: Narudia (anasoma hati ya mashtaka) sasa bwana Kamishna Msaidizi wa Polisi, kama kuna neno Serikali nimelitaja.
Lissu: Waheshimiwa majaji, naomba shahidi ajibu kwa jinsi ninavyomuuliza.
Jaji Ndunguru: Kama shahidi anasema yapo, na wewe unasema hayapo, na hati ya mashtaka mahakama inayo, basi mahakama yenyewe ndiyo ina wajibu wa kujua kama yapo au hayapo.
Lissu: Naomba shahidi ajibu kama kuna maneno Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Kinondoni, Ubungo, Temeke, kama yapo kwenye hati ya mashtaka.
Shahidi: Hayapo… hata Manispaa ya Kigamboni hakuna.
Lissu: Waeleze majaji kama kwenye kosa la uhaini kuna maneno ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Lissu: Waambie kama katika maneno ya kihaini kuna maneno Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango, yapo au hayapo?
Lissu: Kama katika hayo maelezo yanayodaiwa kuwa ni uhaini kuna cheo chochote cha kiongozi wa ngazi yoyote ya kiserikali?
Shahidi: Hakuna cheo cha kiongozi yoyote kwa ngazi yoyote.
Lissu: Katika hayo maneno kama kuna jina la mamlaka yoyote ya kiserikali ya ngazi yoyote, mfano Mtaa wa Mchafukoge, kama yametajwa kwenye hati ya mashtaka?
Lissu: Shahidi, waeleze iwapo katika hayo maelezo yanayodaiwa kuwa ni uhaini, kama kuna Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Shahidi: Serikali inatokana na neno la Kiajemi, ambalo maana yake ni mamlaka au ni watu na taasisi ndani ya jamii zenye mamlaka ya kiutawala. Pia, kunakuwa na kanuni ambazo zinafuatwa kwa ajili ya kulinda kanuni na taratibu zilizopo.
Lissu: Unafahamu kuhusu serikali ya ndani ya Katiba?
Lissu: Naomba usome Ibara ya 151(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Shahidi: Serikali maana yake ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na mtu yeyote anayetekeleza mamlaka kwa niaba ya Serikali.
Lissu: Naomba uwaeleze majaji, aliyekuelekeza kufungua jalada la uhaini alikuwa ni DCI, Ramadhani Kingai na DCP, Ramadhani Ng’anzi.
Shahidi: Sikuelekezwa, mimi mwenyewe nilifungua baada ya kuona upelelezi unajitosheleza.
Lissu: Katika miaka 22 ya kufanya kazi Jeshi la Polisi, umefanya uchunguzi kwenye kesi kubwa ngapi za kisiasa au zenye umuhimu kwa umma kama hii?
Shahidi: Nimewahi kufanya kesi nne.
Shahidi: Ya Dk Willibrod Slaa.
Lissu: Eeh! Ile ya kuchapisha taarifa za uongo, iliishia wapi?
Shahidi: Sijui ilipoishia. Nyingine ni ya Lembeli kule Kahama.
Lissu: Wakati akiwa mbunge au baada ya ubunge?
Shahidi: Huyo Lembeli alikuwa ni public figure (mtu maarufu)?
Lissu: Sijui unatumia kigezo gani? Ulishafanya uchunguzi kesi ngapi za mtu muhimu na mkubwa kwenye siasa kama Tundu Lissu?
Shahidi: Zipo nne, ikiwamo ya John Heche kule Tarime.
Lissu: Eeh! Hiyo ya Heche ulichunguza halafu ikaishia wapi?
Shahidi: Ilifutwa kwa Nolle (kwamba aliyeifungua haendelei na kesi).
Lissu: Katika kazi yako ndani ya miaka 22 ukiwa ofisa wa Polisi, hakuna kesi yoyote uliyochunguza na ikafikia mwisho na mahakama ikatoa hukumu?
Lissu: Hakuna kesi yoyote uliyochunguza ikafikia mwisho, yaani ikatolewa hukumu, ukiachana na hii ambayo ipo hapa mahakamani?
Shahidi: Hakuna, ila ya Tundu Lissu itafika mwisho.
Lissu: Kwa ufahamu wako, kwa nini unasema maneno niliyosema siku ile ya kuita waandishi wa habari yalikuwa ni kosa la uhaini?
Shahidi: Ndiyo, yalikuwa ya kosa la uhaini.
Lissu: Hata wewe Polisi, kuita waandishi wa habari wakusikilize ni kosa la uhaini?
Lissu: Lengo la uhaini lazima lionekane kwa matendo au machapisho au mchoro.
Lissu: Aliyepeleka hayo maneno kwenye mtandao wa Jambo TV ni shahidi P?
Lissu: Aliyerusha maneno hayo kwenye mtandao ni P (shahidi anayelindwa kisheria)?
Shahidi: Ni P na Tundu Lissu.
Lissu: Sasa kwa nini P hajashtakiwa?
Shahidi: Hajashtakiwa kwa sababu ni mwandishi wa habari na hakuja kwako kwenye mkutano wako ili taarifa akaweke jikoni kwake. Huyo P alitueleza baada ya mkutano wa Mwenyekiti wa Chadema, waandishi walitolewa nje ya ukumbi.
Lissu: Huo mkutano na waandishi wa habari ulifanyikia wapi, Mikocheni?
Lissu: Wewe ofisa mzima wa Polisi hujui mkutano ulifanyika wapi, na ndiyo umepeleleza kesi hii?
Lissu: Ulimhoji John Mnyika, Ofisa Habari wa Chadema, Brenda Rupia, juu ya utaratibu wa kualika waandishi wa habari?
Lissu: Waeleze majaji kama mlihoji viongozi wengine wa chama (Chadema) kuhusu utaratibu wa kualika waandishi wa habari.
Lissu: Ila mimi ndiyo umening’ang’ania?
Lissu: Waeleze majaji kama mimi ni mmoja wa wakurugenzi wa Jambo TV.
Shahidi: Sina uhakika wa hilo.
Lissu: Waeleze majaji kama mimi, Tundu Lissu, nina password ya mtandao wa Jambo TV.
Shahidi: Siwezi kufahamu.
Lissu: Kama unajua nina password, waeleze majaji jinsi nilivyoingia kwenye mtandao wa Jambo TV na kuweka hizo picha mjongeo.
Lissu: Waeleze majaji kama wakati unaandika maelezo uliomba ushauri kwa wanasheria.
Shahidi: Sikuomba ushauri.
Lissu: Nani aliyekuambia unaruhusiwa kujiandikia maelezo yako ya onyo mwenyewe?
Shahidi: Hakuna sheria wala kifungu kinachonizuia kuandika maelezo yangu.
Lissu: Nani aliyekukanya?
Shahidi: Sheria ndiyo iliyonikanya.
Lissu: Shahidi, naomba ujibu swali langu, nani aliyekukanya?
Shahidi: Mimi mwenyewe ndiyo niliyejikanya.
Lissu: Nani aliyekuthibitishia hayo maelezo yako uliyoandika?
Shahidi: Mimi mwenyewe, kwa sababu hakuna sheria inayonizuia.
Lissu: Tangu nimetoka JKT, nimeajiriwa na JKT?
Shahidi: Hujaajiriwa, lakini wewe ni askari wa akiba.
Lissu: Hawa askari wa akiba wana masharti sawa na wengine kujiunga na vyama vya siasa?
Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi kesho, Oktoba 8, 2025, ambapo Lissu ataendelea kumhoji maswali ya dodoso shahidi huyo.