Kulia ni mgombea Ubunge Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula na kulia ni mhandishi wa Wakala wa barabara mjini na vijijini, Ernest Nyanda.
Wa kwanza mbele ni mgombea Ubunge Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula,akikagua daraja la miti
……………….
CHATO
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo mkoani Geita, Paschal Lutandula, ameahidi kujenga Daraja la Nyamasenge lililopo kitongoji cha Msasa A kata ya Makurugusi ili kuondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi.
Inaelezwa kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutasaiadia kuinua uchumi wa wananchi wa kijiji cha Imaramawazo kilichopo Jimbo la Chato kusini na kijiji cha Isima Kata ya Nyakagomba Jimbo la Katoro wilayani Geita.
Akizungumza katika ziara ya kampeni za Ubunge kwenye Jimbo la Chato Kusini kwenye Kata ya Makurugusi, Lutandula amesema iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo, atahakikisha anaondoa adha ya wananchi wa kata hiyo kuvuka kwenye daraja la miti na kwamba wananchi hao watajengewa daraja la kisasa ili kunusuru vifo vya wananchi.
Amesema kamwe hawezi kukubali kuona wananchi wa Jimbo lake wakiendelea kupoteza maisha kutokana na ubovu wa daraja hilo na kwamba miezi michache baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge atahakikisha wananchi hao wanafurahia maisha yao kwa kuvuka salama katika eneo hilo.
Ni baada ya baadhi ya wananchi wa kata hiyo kumwomba asaidie kutatua kero iliyodumu tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 ambapo baadhi ya wajawazito na watoto wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kusombwa na maji ya moto lilipo daraja hilo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Imaramawazo, Lushinge Maige, amesema wananchi wa kijiji chake wamekuwa wakishindwa kusafiri kwenda kijiji cha Isima kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara na kwamba baadhi yao hushindwa kuvusha mazao yao kutokana na kudaiwa fedha nyingi.
Kutokana na hali hiyo, mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, akalazimika kuahidi kununua mitambo ya kuchonga barabara itakayoshirikiana na Wakala wa barabara mijini na vijijini(Tarura) kufungua barabara mpya na kukarabati zilizopo ili zipitike wakati wote.
Kwa upande wake msimamizi wa daraja la miti, John Luhemeja, amesema wananchi wanatozwa kiasi cha shilingi 1,000 kila mmoja ili kuchangia gharama za kukarabati miti inayotumika kusimika na kutandaza kwenye kivuko hicho ili kupunguza adha ya wananchi kushindwa kwenda upande wa pili wa wilaya ya Geita.
Hata hivyo, Mhandisi wa barabara za mjini na vijijini(Tarura) wilaya ya Chato, Ernest Nyanda, amesema Ofisi yake imefanikiwa kuitazama kero ya wananchi wa eneo hilo na kwamba baada ya mwaka wa fedha kukamilika daraja hilo litaanza kujengwa haraka kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Mwisho.