Mgombea wa CCM Mabibo atangaza neema lukuki

MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Mabibo, wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam,  kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ashura Mohammed  Seg’ondo, amewataka wananchi katika kata hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu kumpigia kura Mgombea  Urais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na yeye kwa nafasi ya udiwani  ili kuwaletea maendeleo ya haraka.

Aidha amewataka kumchagua Mgombea Ubunge  kwa tiketi ya CCM  katikaJimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo  hali itakayo harakisha maendeleo katika kata hiyo.

 Akihutubia mkutano wa kampeni  katika kata hiyo,  Ashura alisema akichaguliwa  kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha  anasimamia kikamilifu  ujenzi wa miundo mbinu.

“Miundombinu nimeigawanya katika sehemu  mbili. Barabara kuu na barabara za ndani. Katika Mtaa wa Jitegemee  mkandarasi  tayari  anaendelea na ujenzi wa Barabara ya Binti Kayenga. Nami kwa kushirikiana na nyie nitahakikisha kwa ujasiri wangu mkubwa kwa nguvu zangu zote mkandarasi afanye kazi kwa haraka kukamilisha ujenzi,”ameeleza  Ashura.

 Amebainisha,   Kata ya Mabibo, imejaaliwa viwanda  vikubwa hivyo  kwa kushirikiana na viongozi atahakikisha  kwa asilimia kubwa  wakazi wa kata hiyo watananufaika na  ajira.

“Pia katika sekta ya michezo nitahakikisha  tunashirikiana vyema  ili iwe fursa ya ajira kwa sababu Kata ya Mabibo ni  ni kitovu cha mchezo wa  ngumi.  Bondia Mfaume Mfaume anatoka katika   kata hiii,”ameeleza.

Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri , Ashura ameeleza atahakikisha inawasikia walengwa.

“Mikopo inakuja lakini haiwanufaishi walengwa. Nikichaguliwa nitahakikisha mikopo hii inawafikia walengwa. Inawanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kausha damu itakuwa baibai,”ameeleza mgombea huyo.

Amesema atafanya jitihada kuleta walimu wa vikoba kutoa elimu  kwa wananchi katika kata hiyo ili viinue uchumi hasa wawanawake.