MTIA NIA UBUNGE AMFANANISHA MGOMBEA NA HAYATI RAIS DKT. MAGUFULI

Wa kwanza Kushoto ni mtia nia ya Ubunge Jimbo la Chato Kusini CCM, Malale Sende, akimnadi mgombea Ubunge Paschal Lutandula(Hayupo katika picha)

…………..,…

CHATO

ALIYEKUWA mtia nia wa nafasi ya Ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Chato Kusini, Malale Sende, amesema mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, Paschal Lutandula, ndiye pekee anayeweza kuvaa viatu vya aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo cha Chato na rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Amesema mgombea huyo anasukumwa na uzalendo,utashi na utu wa kuwatumikia wananchi na kwamba wananchi hawana budi kumpigia kura nyingi ifikapo Oktoba 29, 2025.

Alikuwa katika mkutano wa kampeni za Ubunge kwenye Kitongoji cha Nyambogo,kijiji cha Mabila kata ya Makurugusi wilayani Chato mkoani Geita huku akiwataka wananchi kutambua kuwa maendeleo ya kweli yatapatikana chini ya Chama Cha Mapinduzi pekee.

Khamis Ndaki (72) amemwomba mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, kuondoa kero ya upatikanaji wa maji ya bomba, kukamilishwa kwa ujenzi wa Zahanati ya Mabila,ujenzi wa Sekondari pamoja na ujenzi wa barabara zinazounganisha vijiji na vitongoji.

Amesema ukosefu wa maji ya bomba umesababisha baadhi ya wananchi kutumia gharama kubwa kutibia magonjwa ya mlipuko na wengine kupoteza maisha kutokana na kutumia maji ya madimbwi ambayo pia hutumiwa na mifugo.

Kwa upande wake Mgombea wa Ubunge katika Jimbo hilo, amesema aslimia 10 ya mikopo ya vijana atahakikisha inafika kijiji cha Mabila ndani ya siku 100 za Ubunge wake na kwamba atahakikisha kiasi cha bilioni 200 zinazotolewa na rais Samia kwa mikopo ya akina mama inawafikia ili kuboresha maisha yao.

Mbali na hilo, amedai atahakikisha vijana wanapata fursa ya kuwa na matamasha mbalimbali ili kuchechemua burudani katika Jimbo lake ikiwemo Ligi ya mpira wa miguu ya Samia Cup.

Hata hivyo amesema ipo changamoto ya Sekondari katika kijiji hicho na kwamba ndani ya siku 100 za utumishi wake atahakikisha shule hiyo inakamilika ili watoto wao wasitembee umbali mrefu kwenda kusoma shule ya Sekondari Kasala na kwamba adha hiyo itabaki kuwa historia.

Aidha kupitia mfuko wa Jimbo la Chato Kusini, atahakikisha ujenzi wa barabara ya changarawe unaanza kujengwa kuanzia kijiji cha Mabila, kuelekea vijiji na kata zingine kwa madai ana nia ya kuwaletea maendeleo ya haraka wananchi wa Jimbo hilo.

Kadhalika hakusahau suala la umeme katika vitongoji vyote vya Jimbo hilo, ikiwemo ukamilishaji wa Zahanati na suala zima la uvuvi wa samaki.

                        Mwisho.