Mtoto wa miaka 11 alivyomuua mwenzake kulipiza kisasi

Iringa. Ni matukio nadra kutokea katika jamii lakini ndivyo ilivyotokea, mtoto Renick Mligo (11) alimuua mtoto mwenzake wa miaka miwili ili tu kulipiza kisasi kwa mama wa marehemu kwa kuwa alimchapa siku kadhaa nyuma.

Mtoto huyo wa kike alimchukua Dafrosia Mwageni (2)na kumpeleka kwenye msitu wa misonobari, akamtundika na kusababisha kifo chake, sababu ikiwa ni kulipiza kisasi kutokana kuchapwa na mama wa marehemu ambaye alikuwa akimlea.

Tukio hilo lilitokea Julai 26,2019 kijiji cha Mahere kilichopo Wilaya ya Njombe wakati huo Renick akiwa na umri wa miaka 11 lakini wakati hukumu ya rufaa yake inatolewa jana Oktoba 6,2025 alikuwa na umri wa miaka 17.

Kwa mujibu wa sheria, adhabu ya kifo haiwezi kutamkwa au kuandikwa dhidi ya mtu yeyote ambaye, wakati wa kufanya kosa alikuwa chini ya umri wa miaka kumi 18, basi mahakama imeamua mtoto huyo awekwe kizuizini.

Kifungu cha 26(2) cha Kanuni ya Adhabu kinasema badala ya adhabu ya kifo, basi mahakama itamuhukumu mtu huyo kuwekwa kizuizini kwa msamaha wa Rais, na ikiwa atahukumiwa hivyo atawajibika kuzuiwa katika sehemu hiyo.

Kuwekwa kwake kizuizini kutafanywa chini ya masharti ambayo waziri mwenye dhamana juu ya mambo ya sheria na sasa Katiba na Sheria atakavyoamuru, na akiwa katika kizuizi hicho atahesabiwa kuwa katika uangalizi halali.

Machi 22, 2022 mbele ya Hakimu Mkuu mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Liadi Chamshama akiwa na mamlaka ya nyongeza, alisikiliza shauri hilo la mauaji dhidi ya Renick aliyetuhumiwa kumuua mtoto mwenzake pia wa kike.

Aliposomewa shtaka la kuua kwa kukusudia, alikiri kutenda kosa hilo ndipo Hakimu Chamshama akamtia hatiani na kumuhukumu kupitia kifungu hicho cha 26.

Maelezo ya kosa ni kuwa Renick alikuwa ni mtoto yatima aliyekuwa akilelewa na mama wa marehemu na kwa sababu fulani isiyoeleweka vizuri, Julai 26,2019 alimchukua mtoto wa mlezi wake na kumpeleka katika msitu wa misonobari.

Huko alimtundika juu na kusababisha kifo cha mtoto huyo na katika kukiri kosa hilo, alieleza kuwa alifanya hivyo ili kulipiza kisasi dhidi ya mlezi wake ambaye alidaiwa alimpiga siku chache zilizopita kabla ya tukio hilo la mauaji.

Tukio hilo la mauaji liliripotiwa polisi siku iliyofuata ambapo mtuhumiwa aliwapeleka polisi hadi eneo la tukio ambapo mwili wa marehemu ulipatikana, mtuhumiwa alihojiwa na polisi na kukiri kumuua mtoto mwenzake.

Mbali na kukiri wakati akihojiwa na polisi, lakini alipofikishwa mbele ya mlinzi wa amani alikiri tena na ndipo alifikishwa mahakamani ambako nako alikiri na kutiwa hatiani na hakimu akaamuru awekwe kizuizini kwa mujibu wa sheria.

Alivyokata rufaa na kukataliwa

Hakuridhika na hukumu hiyo, na kupitia kwa wakili Moses Ambindwile akakata rufaa akiegemea sababu mbili za rufaa lakini hata hivyo jopo la majaji watatu, Lugano Mwandambo, Issa Maige, Latifa Mansoor, wameitupa rufaa hiyo.

Katika hukumu yao iliyotolewa jana Oktoba 6, 2025, walizikataa sababu za rufaa na kueleza kuwa Hakimu Chamshama alikuwa sahihi katika hukumu yake.

Wakili Ambindwile alisema mazingira ya kesi hiyo hayakustahili kufikia hatua ya kumtia hatiani mrufani licha ya kuwa alikiri maelezo aliyosomewa, kwani haiko wazi kama alielewa asili (nature of the offence) ya kosa hilo la mauaji.

Hata hivyo, wakili wa Serikali, Xaveria Makombe ambaye alimwakilisha mjibu rufaa ambaye ni Jamhuri, aliiomba mahakama kutupilia mbali sababu hiyo akisema haikuwa na mashiko kwani mrufani alisomewa maelezo ya kosa na kuyakubali.

Katika uamuzi wao kuhusiana na mabishano hayo, majaji hao walirejea kile kilichotokea mahakamani wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo na kueleza kuwa hata wakili wake hakukosoa utaratibu uliotumika hadi kukiri kosa hilo.

“Kwa kweli, tunashangazwa na hoja ya wakili wa mrufani kwamba mrufani hakuelewa asili ya kosa na kile alichosema baada ya kusomewa shtaka hilo. Kwa heshima, rekodi zinazungumza wazi kabisa.

“Kwanza, akiwa ni mtoto mdogo, mrufani aliambatana na ofisa ustawi wa jamii katika mwenendo wa shauri na kuwakilishwa na wakili,”walisisitiza.

Majaji hao walisema hata aliposomewa maelezo ya kosa alijibu “ni kweli”, hivyo hakuna ubishi kuwa kwa kujibu ni kweli alielewa kuwa anakiri kosa.

Katika sababu ya pili, mrufani alilalamika kuwa hakimu alikosea kisheria na kimantiki kwa kumuhukumu mrufani na kumpa adhabu kinyume cha kifungu cha 26(2),(3), (4) na (5) cha kanuni ya adhabu na kufanya hukumu kuwa batili.

Bila kuweka kesi ya msimamo wa kisheria kuunga mkono hoja yake, wakili Ambindwile kwa nguvu alijenga hoja kuwa katika kutoa adhabu, hakimu alikiuka kifungu cha 26(2) na (3), hoja iliyopingwa vikali na wakili Makombe.

Majaji walikubaliana na hoja ya wakili Makombe kuwa hoja hiyo haina msingi na kunukuu kifungu hicho cha sheria kinavyosema neno kwa neno.

Kifungu kidogo cha (2) kinasema adhabu ya kifo haitatamkwa au kuandikwa dhidi ya mtu yeyote ambaye, wakati wa kufanya kosa mtu huyo alikuwa chini ya umri wa miaka 18, lakini badala ya hukumu ya kifo, mahakama itamuhukumu   kuwekwa kizuizini wakati wa msamaha wa Rais, na ikiwa atahukumiwa hivyo atawajibika kuzuiwa katika sehemu hiyo na chini ya masharti ambayo waziri mwenye dhamana juu ya mambo ya sheria atakavyoamuru, na wakati akiwa katika kizuizi hicho atahesabiwa kuwa katika uangalizi halali.

Pia kifungu kidogo cha (3) kinasema pale ambapo mtu amehukumiwa kuwekwa kizuizini wakati wa msamaha wa Rais kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2), jaji anayesimamia kesi hiyo atapeleka kwa waziri mwenye dhamana juu ya mambo ya sheria nakala ya maandishi ya ushahidi uliochukuliwa katika mwenendo wa kesi, ikiwa na ripoti ya maandishi yaliyosainiwa na yeye na yenye mapendekezo au maoni juu ya jambo hilo kama atakavyoona inayafaa kufanya.

Majaji hao walisema vifungu hivyo vinaeleza kinyume kabisa na kile ambacho wakili Ambindwile alieleza mbele yao na kusisitiza kuwa wajibu wa mahakama ni kutoa adhabu stahiki na sio vinginevyo, tena kwa mujibu wa sheria.

Walisema kinyume na hoja ya wakili Ambindwile, vifungu vidogo vinavyofuata vinahusu utekelezaji wa hukumu ambayo haiwezi kuwa msingi wa rufaa hivyo kwa ujumla wake, majaji walisema rufaa hiyo haina mashiko hivyo inatupwa.