Dar es Salaam. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kuwa wananchi wa Kigamboni hawatolipia tena kivuko iwapo watamchagua kuwa Rais Oktoba 29, 2025.
Amesisitiza kwamba changamoto ya usafiri wa vivuko vinavyotumika kuingia na kutoka Kigamboni jijini Dar es Salaam, ni suala linalogusa maisha ya kila siku ya maelfu ya wananchi wanaotegemea usafiri huo.
Hivyo, amesema Serikali ya chama hicho italivalia njuga suala hilo kwa kusimamia ili kuleta unafuu wa maisha kwa wana Kigamboni.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 7, 2025 akiwa eneo la Feri, Kigamboni kwenye mikutano ya kampeni, Mwalimu amesema haoni sababu ya Watanzania kuendelea kutozwa gharama za kuvuka.
“Sijawahi kuamini wananchi wa Kigamboni kulipia gharama za kuvuka kivuko. Jambo hili linaniuma kama Mtanzania. Hata mimi nikivuka nalipia, inaniuma. Nikichaguliwa suala la wananchi kulipia gharama ya vivuko itakuwa historia, gharama zote zitatolewa na Serikali hii ni huduma kama huduma zingine,” amesema.

Mbali na hilo, Mwalimu ambaye ni katibu mkuu wa Chaumma, ameahidi kuboresha huduma za usafiri Kigamboni kwa kuhakikisha Serikali ya chama hicho inanunua kivuko kikubwa cha kisasa, ili kurahisisha safari za kuingia na kutoka Kigamboni.
Akitolea mfano wa mataifa mengine, amesema hata katika nchi kama Uganda, malipo ya kutumia madaraja huwekewa utaratibu maalumu, huku akijiuliza sababu ya Watanzania kulipia kivuko cha Kigamboni kulipiwa ilhali madaraja kama ya Wami, Maragarasi, Tanzanite na Pangani, yaliyogharimu fedha nyingi, hayalipiwi.
“Kinachofanyika Kigamboni ni uonevu, siamini wananchi wa Kigamboni kulipia Kivuko ili wavuke, nitarekebisha hilo,” amesema.
Kuhusu daraja la Mwalimu Nyerere, Mwalimu amesema serikali ya Chaumma itakuwa tayari kulipa madeni yote ya kivuko kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi, ili wavuke bure.
Pia, amesema Serikali yake ikiingia madarakani atamtaka mfanyabiashara Bakhresa ambaye kwa sasa anahusishwa na huduma ya vivuko Kigamboni, kuwasilisha stakabadhi zake za madai alipwe ili wananchi wasibughudhiwe.
“Hatuna ugomvi na mfanyabiashara yeyote, au mwekezaji. Lakini tunasema huduma ya kivuko ni ya msingi kama shule na hospitali, si haki wananchi kuendelea kubeba mzigo huu,” amesema.
Mbali na hilo, Mwalimu ameahidi kuifufua Kigamboni City, mpango wa maendeleo uliokwama kwa muda mrefu, na kuja na mpango kabambe wa upangaji na upimaji wa ardhi, ili kupendezesha Kigamboni na Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla.
Kwa upande wake, Yericko Nyerere, mgombea ubunge Kigamboni kupitia Chaumma, ameahidi mageuzi makubwa ya maendeleo katika jimbo hilo endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge katika uchaguzi ujao.
Nyerere amesema kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kusuka mtandao wa barabara ndani ya jimbo hilo, akisisitiza kuwa Kigamboni ni eneo lenye utajiri wa madini ya ujenzi lakini miundombinu ya usafiri bado ni changamoto.

“Tutaanza na barabara, haiwezekani eneo lenye uzalishaji mkubwa wa madini ya ujenzi liwe na miundombinu duni. Hatutakubali tena,” amesema Yericko.
Vilevile, amesema ajenda ya pili, ni utatuzi wa changamoto ya vivuko vya feri ambayo amesema imekuwa kero kwa wakazi wa Kigamboni kwa muda mrefu kwa kuwa huduma hiyo ni haki ya msingi kama huduma nyingine na wananchi.
“Huduma ya kivuko ni ya kijamii. Wananchi hawapaswi kulipia kivuko wala daraja la Mwalimu Nyerere kwa kuwa tayari wanalipa kodi. Tukipewa dhamana, hili tutalitekeleza mara moja,” amesisitiza.
Katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi, Yericko amezungumzia mfuko wa jimbo akisema fedha hizo zitarudi kwa wananchi kupitia makundi kama ya waendesha bodaboda na mama lishe.
Amesema kila atakayesajiliwa rasmi atapatiwa leseni pamoja na bima ya afya.
Amesema: “Tutahakikisha fedha za mfuko wa jimbo hazikai ofisini. Bodaboda, mama lishe, wote mtahusishwa rasmi na mtapewa huduma stahiki baada ya kusajiliwa.”
Kwa upande mwingine, Yericko ametaja migogoro ya ardhi kama moja ya matatizo sugu yanayolikabili jimbo hilo na kuahidi kuja na utaratibu madhubuti wa kumaliza migogoro hiyo, ikiwemo kuhakikisha nyaraka za umiliki wa ardhi zinasainiwa na watu wasiopungua saba ili kudhibiti udanganyifu.