CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimekuwa Taasisi ya kwanza nchini Tanzania kupata cheti cha uidhinishaji kutoka European Union Aviation Safety Agency (EASA) Part-66 , kinachokiwezesha kutoa mafunzo na kufanya mitihani ya leseni za wahandisi wa matengenezo ya ndege kwa viwango vya kimataifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho leo, Oktoba 7, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, amesema uzinduzi wa kituo hicho nchini ni hatua ya kihistoria katika kujenga uwezo endelevu wa kitaifa sekta ya anga.
Msangi aliongeza kuwa mafanikio hayo yanadhihirisha dhamira ya serikali kuhakikisha usalama na ufanisi katika usafiri wa anga unakidhi viwango vya kimataifa.
“Kituo hiki ni hatua muhimu katika kujenga uwezo endelevu wa kitaifa katika usalama na uhandisi wa usafiri wa anga. TCAA itaendelea kuhakikisha mafunzo na mitihani inayoendeshwa NIT inakidhi viwango vya EASA na inaleta ulinganifu katika eneo la Afrika Mashariki kupitia EAC-CASSOA,” alisema Msangi
Hatua hii ni ya kihistoria katika maendeleo ya mafunzo ya anga nchini.” Amesema
“Kituo hiki kinathibitisha uongozi wa Tanzania katika usalama wa anga na ubora wa mafunzo. Ni hatua ya kimkakati kuelekea kujenga uwezo endelevu wa kitaifa na kupata utambuzi wa kimataifa,” alisema Msangi.
Alifafanua kuwa kituo hicho kimejengwa kupitia uwekezaji wa dola milioni 21.25 za Marekani chini ya mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, wenye lengo la kukibadilisha NIT kuwa kituo cha ubora wa juu cha kikanda katika mafunzo ya anga na usafiri.
Kwa kushirikiana na Athens Aviation Training Organization (AATO) kutoka Ugiriki, kituo hicho kimejengwa kwa kuzingatia viwango vya EASA Part-66 vinavyotambulika duniani kote katika utoaji wa leseni za wahandisi wa matengenezo ya ndege.
Msangi aliongeza kuwa TCAA imeidhinisha NIT kupanua wigo wa mafunzo yake kujumuisha mafunzo ya marubani, uendeshaji wa safari za ndege, mafunzo ya wapangaji safari (dispatchers) na mafunzo ya wahudumu wa ndani ya ndege (cabin crew).
“Kuongeza mafunzo haya kutaiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu cha elimu ya anga kwa ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Msangi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, alisema cheti hicho ni mafanikio makubwa kwa taifa na taasisi hiyo.
“Tumegeuza uwekezaji kuwa fursa. Uidhinishaji huu wa EASA unawawezesha wanafunzi wetu kupata sifa za kimataifa wakiwa nyumbani, na kuifanya NIT kuwa kitovu cha ubora wa mafunzo ya anga kwa Afrika Mashariki na Kati,” alisema Dkt. Mgaya.
Dkt. Mgaya alibainisha kuwa tayari wakufunzi nane wa Kitanzania wamepata vyeti vya kufundisha kwa viwango vya EASA, huku wengine wakiendelea na mafunzo katika moduli 17 tofauti kwa udhamini wa NIT.
Kituo hicho kipya kina miundombinu ya kisasa ikiwemo vyumba vya madarasa vya kidigitali, ndege za mfano kwa mafunzo (mock-up aircraft), vifaa vya kisasa vya majaribio na simulators za mafunzo ya kuruka na matengenezo, pamoja na maabara za hali ya juu zinazokidhi matakwa ya viwango vya kimataifa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa Aerolink Solutions Tanzania Mhandisi Edith Kisamo, ambaye ni mmoja wa wadau wakuu wa sekta binafsi katika mradi huo, alisema uzinduzi huo ni “kuruka kihistoria” kwa maendeleo ya viwanda na vijana nchini.
“Mafanikio haya yanaonyesha kuwa viwango vya kimataifa vinaweza kufikiwa na Watanzania wenyewe kupitia vipaji vya ndani. Wahandisi wetu sasa watapata mafunzo, leseni na ajira hapa hapa Afrika,” alisema.
“Kupitia ushirikiano huu, Aerolink imeunganisha utaalam wa kimataifa na ndoto za Kitanzania kuhakikisha kizazi kijacho cha wahandisi kinapata mafunzo, vyeti, na ajira hapa hapa Afrika,” alisema.
Aliongeza kuwa, Tanzania ikijiandaa kwa ukaguzi wa usalama wa anga wa kimataifa (ICAO Universal Safety Oversight Audit – USOAP) mwaka 2026, kituo hicho kitakuwa chachu muhimu katika kuimarisha ufanisi wa udhibiti, kupunguza utegemezi wa mafunzo nje ya nchi na kuongeza ajira zenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya anga.
Kwa upande wake, Georgios Samiotis, Mkurugenzi Mtendaji wa AATO kutoka Ugiriki, alisema mafanikio hayo ni mfano wa namna uwekezaji wa Ulaya unavyoweza kujenga uwezo wa Afrika na kuimarisha ukuaji endelevu wa sekta ya usafiri wa anga.
“Kupitia hatua hii, wakufunzi nane (8) wa Kitanzania kutoka NIT wameidhinishwa rasmi na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Ugiriki (HCAA) kuwa walimu wa kwanza wa EASA katika Afrika Mashariki. Hii ni hatua kubwa kuelekea kujenga Center of Excellence ya mafunzo ya anga barani Afrika.” Alisema
Kituo hiki kinatazamiwa kuchochea ajira, kuongeza ujuzi wa vijana, na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, hususan katika eneo la matengenezo na ukarabati wa ndege (MRO).
Kulingana na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), bara la Afrika litahitaji zaidi ya wahandisi wa ndege 55,000 kufikia mwaka 2040. Kupitia uwekezaji huu, Tanzania imejiweka katika nafasi bora ya kushiriki kikamilifu katika soko hilo la ajira na maendeleo ya teknolojia ya anga.