Unguja. Mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT – Wazalendo, Othman Masoud Othman amedai kuwa hoja kuhusu mustakabali wa kisiwa hicho, zinazotolewa kwenye mikutano yake ya hadhara zinafuatiliwa na watu wengi.
Amefafanua kuwa kila hoja wanayoizungumza kwenye mikutano yao ya kampeni inayorushwa mbashara kupitia mitandao ya kijamii, zimekuwa mjadala mitaani akisema pia wanapata salamu kila pembe ya dunia.
“Ndugu zangu mikutano yetu inawafanya watu waache kazi watusikilize. Hii ni kwa sababu Wazanzibari wenzetu, wananchi wetu wanatufuatilia, kwa sababu tunazungumza mustakabali wa Zanzibar nchi yao,” amesema.
Othman ameeleza hayo leo Jumanne akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Jimbo la Chwaka, Unguja. Tangu jana Jumatatu, Othman ameendelea na kampeni zake Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kumaliza kisiwa cha Pemba.
Amesema endapo atachaguliwa Oktoba 29, 2025 atahakikisha anaondoa kasoro zote zinazosababisha Wazanzibari kukosa haki za msingi na sabambamba na kuondoa dhuluma ikiwemo hali ngumu ya maisha, umasikini na wananchi kunyang’anywa ardhi zao.
“Hivi wananchi wa Chwaka, hamtaki kutoka katika madhira haya? Kama mnataka sasa kazi ni ndogo Oktoba 29 mpe kura yako Othman Masoud awe rais wa Zanzibar au hamuamini kama naweza kurekebisha haya? Akajibiwa na wananchi ‘tunakuamini’.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa amesema Othman ameshafanya mikutano 20 ya majimbo ya Pemba na Unguja tangu alipozindua kampeni za kusaka urais mwezi uliopita.
Jussa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar), amewahakikishia Wazanzibari kuwa mshahara wa kima cha chini wa Sh1 milioni kwa watumishi wa umma, inawezekana kwa sababu chama hicho kina sera nzuri ya kuwainua watendaji wa Serikali.
“Ndugu zangu wanaMarumbi (Chwaka), tutafanya kampeni bila kuchoka. Tunajua Othman atashinda, lakini tunataka tuandike ushindi ambao haujapata kutokea. Twendeni tukafanye kazi ili tumchague Othman awe rais wa Zanzibar,” amesema Jussa.
Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma ACT Wazalendo, Salim Biman amesema ziara ya mgombea huyo kesho Jumatano Oktoba 8, 2025 itakuwa uwanja wa Magirisi Jimbo la Mwanakwerekwe.
Amewataka Wazanzibari kumpigia kura za wingi Othman ambaye ameahidi kulipa mshahara wa Sh1 milioni kima cha chini, akisema hiyo neema kubwa kwa wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Wafanyakazi wote watapata neema ndani ya Zanzibar, chini ya Othman Masoud Othman ‘OMO’,” ameeleza Bimani ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya ACT Wazalendo.