Pacome awekwa mtu kati na wawili wa Ulaya

STAA wa Yanga, Pacôme Zouzoua ameachiwa zigo huko Ivory Coast mbele ya Simon Adingra wa Sunderland ya Ligi Kuu England na Yan Diomande wa Leipzig ya Bundesliga wakati wakijiandaa na mechi mbili za kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia.

Pacome ambaye hii ni mara ya pili kuitwa kwenye kikosi hicho cha timu ya taifa la Ivory Coast, alikuwa sehemu ya wachezaji 13 ambao walianza mazoezi ya pamoja juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Cocody Technical jijini huko Abidjan huku wengine walitarajiwa kuwasili jana Jumanne na leo Jumatano.

Katika mechi mbili Ivory Coast itacheza ugenini Oktoba 10 dhidi ya Shelisheli na nyumbani dhidi ya Kenya siku nne baadaye ili kujihakikishia kumaliza kinara wa kundi F. Kwa sasa inaongoza ikiwa na pointi 20 ikifuatiwa na Gabon 19.

Kwa Pacome zigo alilo nalo ni kupigania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza upande wa winga ya kulia ambako wapinzani wake wakubwa ni Adingra  ambaye msimu huu akiwa na Sunderland amecheza mechi sita za Ligi Kuu England hajafunga lakini ana asisti moja.

Huyo ndiye mchezaji ambaye amekuwa akicheza mara kwa mara nafasi hiyo na katika fainali zilizopita za Mataifa ya Afrika alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi. Mbali na Adingra, Pacome atakuwa na kibarua kingine mbele ya Diomande ambaye naye ni mgeni timu ya taifa. Diomande ambaye ni kinda mwenye miaka 18, amekuwa kwenye kiwango bora kiasi cha kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Leipzig, amecheza mechi sita hajafunga wala kutoa asisti.

Mbali na ukubwa wa majina ya wachezaji hao pamoja na ligi ambazo wametoka, Pacome anaweza kubebwa na uzoefu wake hasa katika michuano ya kimataifa ambako amekuwa mmoja wa wachezaji hatari, msimu uliopita aliisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa nne mfululizo kwenye ligi akifunga mabao 12 na kutoa asisti 10, akihusika kwenye mabao 22.

Kwa upande wa winga ya kulia wachezaji ambao wanapewa nafasi kubwa ya kutumika ni wale wenye ufanisi mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto akiwemo nyota wa zamani wa Arsenal, Nicolas Pépé ambaye msimu huu akiwa na Villarreal ya Hispania amefunga mabao mawili na kutoa asisti moja katika mechi nane za La Liga.

Mchezaji mwingine ambaye anapewa nafasi kubwa upande wa winga ya kulia ni Amad Dialo wa Manchester United, anaasisti moja katika mechi sita za Ligi Kuu England. Kama Ivory Coast itashinda mechi hizo basi Pacome ataweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kufuzu fainali hizo akiwa na Ivory Coast.