Huko Simba mambo yameanza kwa kasi baada ya ujio wa Dimitar Pantev, ambapo unaambiwa ameshaanza kuwapa hesabu zake mastaa wa timu hiyo namna anavyotaka kukijenga kikosi hicho, huku akipiga mkwara.
Pantev alitua siku chache zilizopita akiwa ndiye mrithi wa kocha Fadlu Davids aliyeondoka baada ya mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United.
Simba ilikutana na Gaborone ya Botswana na mechi hizo mbili kumalizika kwa Wekundu wa Msimbazi kushinda jumla ya mabao 2-1, huku Pantev aliyeiongoza Gaborone akitua kuja kuchukua mikoba ya Fadlu.

Oktoba 6, 2025, Pantev alianza kukinoa kikosi hicho ambapo baada ya kukutana na wachezaji, yapo mambo ambayo amezungumza na mastaa hao.
Beki mmoja wa Simba amefichua kwamba Pantev ambaye ametambulishwa klabuni hapo kama Meneja Mkuu, kwenye mkutano wake wa kwanza na kikosi hicho amewataka wachezaji kujiamini na kuwa jasiri kuipigania timu kwenye mechi zote.
Amesema Pantev anataka kufanya kazi na wachezaji wanaojituma na wanaofuata maelekezo ya namna wanavyotakiwa kutekeleza falsafa zake, huku akisisitiza asiyejituma hana nafasi.
“Huyu ni kocha mzuri. Ametuambia anataka kufanya kazi na wachezaji wanaojituma. Anataka kuona mchezaji akipewa nafasi anaonyesha uwezo kama hataipata tena. Anataka wachezaji tuwe jasiri uwanjani tuipiganie Simba,” amesema beki huyo.

“Anataka kufanya kazi na wachezaji wanaotekeleza majukumu ambayo anatupa uwanjani. Hataki kuona tunatoka nje ya falsafa yake na kila mtu akifanya vizuri atapata nafasi.”
Naye mshambuliaji mmoja wa timu hiyo amefichua zaidi akisema Pantev anataka kuona kikosi kinacheza soka la kushambulia.
Mshambuliaji huyo amesema mkufunzi huyo amewaambia anataka kuona timu inatengeneza nafasi kwenye mechi na kuzitumia, huku wakiwa sawa kwenye ulinzi.
“Falsafa zake anataka kuona tunacheza soka la kushambulia na sio kukaa nyuma, tutengeneze nafasi na sisi washambulaji tuhakikishe tunazitumia.
“Kama nilivyokwambia hataki tukae nyuma ya mpira, lakini anataka umakini kwenye ulinzi, anasema Simba, lazima icheze mpira wa ushindi lakini kuhakikisha mashabiki wanafurahia timu yao kwa kuwa tupo kwa ajili yao,” amesema.

Mtihani wa kwanza kwa Pandev utakuwa ugenini wakati Simba itakaposafiri kuifuata Nsingizini Hotspurs kwenye mechi ya mtoano ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Oktoba 19, 2025.