Mwanza. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi ( CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendeleza mambo mbalimbali ambayo tayari Serikali imeyafanya katika kipindi cha miaka mitano wilayani Misungwi, ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuimarisha huduma za jamii pamoja na biashara katika Jiji la Mwanza.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 7, 2025 baada ya kuwasili katika viwanja vya Misungwi, mkoani Mwanza akitokea Kata ya Buhongwa.
Katika ahadi zake kwa wakazi wa Misungwi, mgombea huyo amesema akichaguliwa kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ataongeza vizimba ili kutoa ajira kwa vijana kujiajiri kupitia Ziwa Victoria, kwa kipindi kilichopita vizimba 400 vimejengwa na tayari vijana wamejiajiri.
Sambamba na hilo, ameahidi ujenzi wa uzio ndani ya Ziwa Victoria kwa lengo la kudhibiti mamba ili kuwalinda wananchi wanaotumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo akina mama wanaojishughulisha na uvuvi.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imejenga vizimba 400 vya kufugia samaki katika mwalo wa Kigongo na kuwa akipewa ridhaa ya kuongoza tena ataongeza vizimba ili visaidie vijana kujiajiri na kuongeza kipato.
“Akina mama wa Mwanza, shughuli zao nyingi ni ziwani ila kuna mamba, tumeanza kujenga uzio ndani ya ziwa ili kuwaweka mamba pembeni na akina mama ili wafanye shughuli zao. Tutaendelea kuweka uzio ili tuwaweke binadamu mbali na hatari ya mamba,” amesema.
Kuhusu ombi la wavuvi kutumia jengo la abiria, lilipokuwa eneo la Feri ya Kigongo kama soko amesema,
“naelewa mnataka soko jipya la kisasa kuuzia samaki, kwa hatua ya sasa hamna kizuizi, halmashauri ifanyie kazi na ninawaahidi tutajenga soko jipya au kuboresha jengo hilo ili liwe na vifaa vya kuhifadhia samaki.
“Mbali na hilo, naahidi tutajenga soko kuu la kisasa Misungwi, stendi ya mabasi madogo na stendi ya mabasi makubwa ili kuchochea shughuli za kiuchumi wilayani humu,” amesema Samia.
Kuhusu miundombinu ya barabara, ameahidi kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ili kuboresha mtandao wa barabara Mwanza.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanaimarisha upatikanaji wa huduma za usafiri na kukuza maendeleo ya kiuchumi katika jiji hilo.
Awali, kabla ya ahadi hizo mgombea huyo alieleza wananchi hao kuwa alipokea nafasi hiyo wakati ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi (JPM) ulikuwa umefikia asilimia 20 ila kwa sasa limekamilika na limepunguza muda wa watu waliokuwa wakiutumia kusafiri na baada ya kukamilika wanatumia muda mchache.
“Leo daraja limekamilika, ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR umefika asilimia 65 na wakati ule marehemu (Hayati John Magufuli) aliacha tunazungumza kuhusu ujenzi wa meli kubwa ya MV Mwanza, sasa inafanya majaribio ziwani, miradi yote mikubwa nimeimaliza,” amesema.