Mwanza. Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amewaahidi wakazi wa Buhongwa kupata maji saa 24 kwa mwaka mzima baada ya kukamilika kwa ujenzi wa matangi matatu ya kuhifadhia maji yanayojengwa katika eneo hilo na maeneo ya jirani.
Samia ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 7, 2025 wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Buhongwa mkoani Mwanza ikiwa ni siku yake ya kwanza kunadi ilani ya CCM, na kuomba ridhaa ya urais kwa miaka mitano ijayo mkoani humo.
Amesema Buhongwa litajengwa tangi la maji lenye ujazo wa lita milioni 10, Fumagila ya juu likijengwa lenye ujazo wa lita milioni 10 na Nyamazobe litajengwa la ujazo wa lita milioni tano.
Amesema licha ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayoendelea, kumekuwa na tatizo la presha ndogo ya maji katika baadhi ya maeneo hasa ya miinuko.
“Sasa kwa maji tumetekeleza mradi mkubwa wa Butimba kwa Sh71.7 bilioni na kuwafikishia maji safi na salama wakazi 450,000 wakazi wa Buhongwa, Nyegezi, Igoma na kwingineko,” amesema mgombea huyo.
Amesema wametekeleza mradi mwingine wa maji wa Sh868 milioni ulionufaisha wakazi wa Sahwa, Buhongwa na Lwanhima huku miradi mingine ikiendelea kutekelezwa kwa Sh462 bilioni eneo la Buhongwa, Kishiri imefikia asilimia 85.
“Ahadi yenu ni kukamilisha miradi hii pamoja na upanuzi wa mradi wa chanzo cha Capripoint ili kuimarisha upatikanaji wa maji. Baada ya kumaliza matangi haya mtiririko wa maji utakuwa mzuri yatapatikana maneno ya vijana saa 24 mwaka mzima,” amesema.
“Kijana wenu (Waziri wa Maji, Jumaa Aweso) nilikuwa namkaba na yuko vizuri, miradi mbalimbali ilitekelezwa ukiwemo mkubwa hapa Butimba,” amesema.
Mgombea huyo amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imetekeleza miradi mingine ikiwemo ya afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Amesema katika eneo hilo la Nyamagana, wameboresha hospitali ya wilaya, ujenzi wa vituo vinne vya afya, shule sita za sekondari, shule nane za msingi pamoja na ujenzi wa mabweni mawili na uzio kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Buhongwa.
Samia amesema Mkoa wa Mwanza ni wa muhimu kwa biashara na shughuli za uzalishaji hasa kilimo na uvuvi na kuwa kipaumbele cha CCM ni huduma za jamii, na Serikali itaendeleza na kukuza nguzo hizo kuu za uchumi zikitanguliwa na maendeleo ya jamii.
Kuhusu uwanja wa ndege Mwanza, mgombea huyo ameahidi kuboreshwa kwa uwanja huo ili uwe wa kimataifa ambapo alitumia nafasi hiyo kuomba kura kwake, wagombea ubunge na udiwani.
Wananchi waliofika kumpokea mgombea urais huyo, wameeleza sababu ya kumwamini Samia, wakitaja mambo aliyoyafanya katika kipindi chake cha miaka minne akiwa Rais baada ya mtangulizi wake, hayati John Magufuli kufariki dunia.
“Mimi sina wasiwasi na Samia, ametufanyia mengi hasa daraja la Magufuli ambalo linatuwezesha na kuturahisishia ufanyaji biashara. Tunaamini mama huyu anajali na ataendelea kutufanyia makubwa,” amesema Maria Saloje, mkazi wa kata ya Buhongwa mkoani Mwanza.