Bunda. Serikali imetoa zaidi ya Sh5 bilioni kuwalipa fidia wakazi 1,298 wa vijiji 29 kutoka wilaya za Bunda mkoani Mara na Ukerewe mkoani Mwanza, kwa ajili ya kupisha utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132.
Mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh136 bilioni unatarajiwa kujengwa kutoka wilayani Bunda hadi Ukerewe umbali wa kilomita 98.6, ambapo umeelezwa kuwa utakapokamilika utaboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika wilaya hizo pamoja na za jirani.
Akizungumza wakati wa ulipaji wa fidia kwa wakazi hao leo Jumanne Oktoba 7, 2025 katika Kijiji cha Kisorya wilayani Bunda, Meneja wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mara, Nickson Babu amesema mradi huo pamoja na mambo mengine unatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu juu ya changamoto ya upatikanaji wa umeme wa kutosha katika maeneo hayo.
“Niwahakikishie walengwa wote wa fidia watapata stahiki zao kwa mujibu wa tathmini na sheria na kwa wale ambao wana changamoto naomba wazilete kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ili zifanyiwe kazi na hakuna mtu atakayetozwa fedha kwa ajili ya kuhudumiwa changamoto yake,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kisorya wilayani Bunda wakisubiri kupokea hundi zao za malipo ya fidia kupisha utekelezaji wa mradi wa umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka wilayani Bunda mkoani Mara kwenda Ukerewe mkoani Mwanza. Picha na Beldina Nyakeke
Babu amesema hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo kwa sasa hairidhishi ingawa unapatikana, hivyo mradi huo pamoja na mambo mengine utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi na wawekezaji kwa ujumla kwani utasaidia kupatikana kwa umeme wa kutosha muda wote.
Ametoa wito kwa walengwa ambao watakuwa mabadiliko ya umiliki wa maeneo baada ya tathmini kufanyika kutokuwa na hofu badala yake wawasilishe nyaraka husika, ili malipo yaweze kufanyika kwa wakati.
“Yawezekana kuna mabadiliko ya umiliki yametokea mfano kuna vifo au unadhani kuna shida kwenye tathmini yako wala usiogope njoo kwa Mtendaji wa Kata ambaye atawasilisha suala lako kwetu, sisi tutayafanyia kazi ndani ya muda mfupi lengo ni kuhakikisha watu wote wanalipwa na mradi unatekelezwa kwa wakati.
Meneja Usimamizi wa Mradi huo, George Uhakula amesema ukikamilika utasaidia kufungua njia za uwekezaji katika maeneo hayo tofauti na sasa ambapo umeme uliopo wa kilovoti 33, hauwezi kuhimili shughuli kubwa za kiuwekezaji.
“Kwa Wilaya ya Bunda mkoani Mara mradi umepitia vijiji 24 na kwa kule Ukerewe ni vijiji vitano ambavyo wakazi wake wanalipwa fidia ili kupisha mradi huu ulioanza kutekelezwa mwaka 2023, na tunaamini yale maoni ya uwekezaji yatatimia kwani sasa kutakuwa na umeme wa kutosha kwani mradi huu ni wa kuzalisha kilovoti 132 tofauti na hizi 33 za sasa,” amesema.
Uhakula amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema Aprili 2026, ambapo mwanzoni ulisimama kwa muda kutokana na changamoto ya fidia jambo ambalo tayari limepatiwa ufumbuzi baada ya Serikali kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya malipo.
Tayari utekelezaji ulikwishaanza na shughuli na kazi za usanifu zimekamilika kwa zaidi ya asilimia 98 huku uboreshaji wa kituo cha kupoozea umeme umefika asilimia 30.2 na ujenzi njia ya kusafirisha umefika asilimia 15.2 . Kwa hiyo tunatarajia mkandarasi kurudi tena eneo la kazi baada ya kumaliza malipo haya ya fidia,”amesema.
“Ukanda huu kuna malighafi ambayo yanaweza kutumika kwenye viwanda kuna samaki, matunda na hata madini hivyo kuwepo kwa umeme mkubwa kutasababisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye sekta hizo,” amesema Mafuta Pamba.
Winfrida Lugela amesema uchumi wa wakazi wa maeneo hayo utaimarika zaidi kufuatia uwepo wa shughuli kubwa za wawekezaji hivyo kuondokana na umaskini.
“Kwanza, baada ya kufanyiwa tathmini hatukutarajia kupata malipo kwa sababu mambo ya Serikali huwa hayaeleweki, lakini tuna furaha kubwa kuwa leo tunapokea malipo yetu ili tupishe mradi uendelee, hii kwetu ni faraja kwani mbali na malipo lakini tunatarajia kupata fursa nyingi za kiuchumi kutokana na uwepo wa umeme wa kutosha,” amesema.