Sh600 milioni kujenga soko la madini Songwe

Songwe. Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani Songwe imeanza ujenzi wa mradi wa soko la madini katika mji wa Mkwajuni, unaotarajia kugharimu Sh600 milioni wenye vibanda 40.

Mradi huo wa ujenzi wa soko la madini, unaotekelezea na halmashauri hiyo kupitia mapato ya ndani, umewekwa jiwe la msingi Oktoba 6, 2025 na kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025, Ismail Ali Ussi.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa soko hilo, ofisa biashara Wilaya ya Songwe, Maria Chacha amesema lengo la kujenga mradi huo ni mpango wa halmashauri kuboresha miundombinu ya biashara ya madini, kuongeza mapato na kutengeneza fursa za ajira.

Amesema mradi huo unatelelezwa na mkandarasi, Okasseny Engineering Limited kwa awamu mbili kwa gharama ya Sh600 Milioni ambapo kwa awamu ya kwanza zimetolewa Sh389.6 milioni ambapo kiasi kilichotumika ni Sh187.9 milioni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya jengo lenye vyumba 40.

“Jengo hilo linatarajia kuwa na vyumba kwa ajili ya biashara, eneo la kusubiria, matundu ya vyoo sita na eneo la usahili na mashimo ya maji taka,” amesema Chacha.

Chacha amesema ujenzi huo unakabiliwa na changamoto tangu kuanza kutekelezwa Mei 15, 2025 ikiwemo umeme, maji ambapo umeshindwa kukamilika kwa wakati uliopangwa Septemba 13, 2025.

Akiweka jiwe la msingi kwenye jengo la soko hilo, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi amesema ujenzi wa soko hilo utaisaidia halmashauri hiyo kujipatia mapato ya kutosha kutokana na mauzo yatokanayo na mauzo ya madini.

Amesema sekta ya madini huliingizia taifa pato ambalo hutumika kuendelezea miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, maji, elimu na hospitali, hivyo ujenzi wa soko hilo litawanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

“Niwaombe wafanyabiashara, mkalitumie soko hili la madini kwani litawarahisishia kuondoa usumbufu mliokuwa mnapata hapo awali, niwasihi pia mlitumie soko hili kulipa kodi kwa maendeleo ya sekta ya madini,” amesema.

Kwa upande wake, ofisa madini Mkoa wa Songwe, Chone Malembo amesema awali wafanyabiashara walikuwa wanapata changamoto ya kuuza madini, hivyo kukamikika kwa ujenzi wa soko hilo kutakuwa mkombozi.

Amesema soko linalotumika sasa lina vyumba 26 ukilinganisha na uhitaji wa wafanyabiashara wa vibanda zaidi ya 50.