Dar es Salaam. Sakata la aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, aliyeripotiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana katika mazingira tata limetua mahakamani.
Mawakili wa Polepole aliyejiuzulu wadhifa huo hivi karibuni wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala wamefungua shauri la maombi maalumu kwa niaba yake, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine wakiomba amri ya mahakama kuwaamuru Wajibu maombi katika shauri hilo kumfikisha mahakamani.
Wajibu maombi katika shauri hilo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polis Kanda Maalum Dar es Salaam (ZPC).
Mawakili wake hao leo Oktoba 7, 2025, wamefungua shauri hilo mahakamani hapo chini ya hati ya dharura wakiomba afikishwe mahakamani.
Katika hati hiyo ya dharura iliyothibitishwa na Wakili Kibatala anaeleza kuwa tangu Jana Oktoba 6, 2025, Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi waliovamia nyumbani kwake Ununio, Wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
Pia, wakili Kibatala anadai kuwa mpaka sasa hajashtakiwa kwa kosa lolote la Jinai katika mahakama yoyote ya kisheria na kwamba inaaminika kuwa amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.
”Hivyo haki zake za Kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi”,amesema Kibatala na kuongeza:
”Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake.”
Katika hati maombi wanaomba wasikilizwe upande mmoja na Mahakama iamiri Polepole afikishwe mahakamani akisubiri uamuI wa maombi hayo kusikilizwa pande zote.
Katika usikilizwaji wa maombi hayo pande zote wanaomba. mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamuachilie huru mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika Mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.