Siri vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura

Dar es Salaam. Kadiri miaka inavyokwenda, mwamko wa wananchi kujitokeza kupiga kura umekuwa ukishuka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo baadhi ya vyama vya siasa kukosa sera bora za kuwavutia wapigakura.

Kwa mujibu wa taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020, kati ya wapigakura 29,754,699 walioandikishwa katika daftari, wapigakura 15,091,950 sawa na asilimia 50.72 ndio walijitokeza kupiga kura.

Katika tathmini ya mwitikio wa wapigakura, jumla ya mikutano na mijadala 24 ilifanyika. Washiriki wa mikutano hiyo walitoka kwenye makundi ya wazee, vijana, watu wenye ulemavu na wanawake.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ambayo sasa inajulikana kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ilibainisha sababu kadhaa zilizosababisha mwitikio mdogo wa wananchi kwenda kupiga kura.

Baadhi ya sababu zilizobainishwa ni pamoja na baadhi ya vyama kununua kadi za wapigakura ili washindwe kwenda kupiga kura, na baadhi ya vyama kushindwa kufanya kampeni za kutosha katika maeneo yote.

Sababu nyingine ni baadhi ya wapigakura kutohakiki majina yao kwenye daftari, hivyo kushindwa kufahamu vituo watakavyopigia kura vilipo, baadhi ya vyama kuwashawishi wapigakura wasiende kupiga kura, na baadhi ya vyama kukosa sera bora za kuwavutia wapigakura.

Ili kuboresha mwitikio wa wapigakura, tume ilipendekeza mambo kadhaa, ikiwemo elimu ya mpigakura iwe endelevu na itolewe kwa muda mrefu zaidi kwa maeneo yote nchini, hasa vijijini, asasi za kiraia na taasisi nyingine zinazohusika na utoaji wa elimu ya mpigakura ziruhusiwe kutoa elimu endelevu.

Pia, ilipendekeza uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura uwe endelevu, watendaji wa tume waendelee kusimamia uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi zao bila upendeleo na tume ianzishe utaratibu wa kupiga kura kwa njia ya mtandao.

Kutokana na changamoto hiyo, vyama vya siasa katika kampeni za uchaguzi mkuu ukaofanyika Oktoba 29, vimejitoa kuhamasisha wananchi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi ili wapate viongozi wanaowataka.

Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi, wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kupitia kaulimbiu yao ya “Oktoba Tunatiki.”

Vyama vingine kama Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kupitia mgombea wake, Salum Mwalimu, na NLD kikiwakilishwa na Doyo Hassan Doyo navyo vimekuwa vikihamasisha wananchi kwenda kupiga kura.

Mwamko huo wa vyama vya siasa kuhamasisha wananchi kupiga kura umewaibua wachambuzi wa siasa ambao wanasema ni mwenendo mpya unaoashiria ama kukua kwa demokrasia au kupungua kwa mvuto wa kisiasa miongoni mwa wananchi kutokana na matokeo ya chaguzi zilizopita.

Mchambuzi wa masuala ya siasa na kijamii, Said Miraj, amesema mwelekeo huo unatokana na vyama kutambua umuhimu wa ushiriki mkubwa wa wapigakura katika kuhalalisha ushindi.

“Kuna sababu mbili kuu, ya kwanza, kila chama kinataka kupata wapigakura, maana bila wapigakura huwezi kuchagulika,” anasema Miraj.

Anasema licha ya wananchi wengi kujiandikisha katika chaguzi zilizopita, idadi ya wanaojitokeza kupiga kura imekuwa ndogo, jambo linalowafanya wanasiasa kubadili mbinu.

“Rekodi zinaonesha watu wengi wanajiandikisha lakini hawapigi kura. Wengine wanajiandikisha ili wapate vitambulisho kwa matumizi mengine. Hivyo, mwaka huu vyama vimeamua kushika bango la kuwahimiza watu wajitokeze kupiga kura,” anafafanua.

Anaongeza kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya vyama vikubwa kutoshiriki uchaguzi wa mwaka huu, hali inayoweza kushusha hamasa.

“ACT-Wazalendo haina mgombea urais na haijatoa maelekezo rasmi kwa wanachama wake. Chadema nao hawashiriki kabisa uchaguzi mkuu. Vyama hivi havitahamasisha watu kupiga kura, jambo linaloweza kushusha idadi ya wapigakura,” anasema.

Miraj anaongeza kuwa tishio la vurugu na maandamano nalo limechangia vyama kubadili msimamo wa kampeni.

“Wapo wanaotishwa kwamba kutakuwa na maandamano siku ya uchaguzi, polisi nao wanasema watayazuia. Wenye roho ndogo wataamua kukaa majumbani, hivyo vyama vinatumia nguvu kubwa kuwahakikishia wananchi usalama,” anasema.

Kwa mujibu wa Miraj, ushiriki wa wananchi kwenye uchaguzi unahalalisha matokeo, na kutoshiriki kunazifanya kura chache kuamua hatima ya nchi, hivyo kiongozi kukosa nguvu ya umma.

“Kwa mfano, waliojiandikisha ni milioni 30, lakini wakapiga kura milioni 12, ukapata milioni saba, utakuwa umeshinda, lakini kidemokrasia ushindi wako hauna mashiko,” anasema.

Kwa upnde wake, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie, anasema mabadiliko ya mwelekeo wa kampeni yanatokana na athari za kampeni ya ‘No Reforms, No Election’ iliyoanzishwa na Chadema.

“Ziko sababu tatu. Kwanza, harakati za Chadema za ‘No Reforms, No Election’ zimewafanya baadhi ya Watanzania waamini kwamba lazima kuwe na mabadiliko kabla ya kushiriki uchaguzi. Hivyo, vyama vingine vinahamasisha watu kupiga kura ili kupunguza athari za wito huo,” anasema.

Sababu ya pili, anasema, ni kupungua kwa imani ya wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi kutokana na changamoto za kampeni na matokeo ya nyuma.

“Watu wamepoteza mvuto kutokana na namna mchakato wa kampeni na matokeo unavyotangazwa,” anasema.

Anaongeza kuwa sababu ya tatu ni kutokuwepo kwa vyama vyenye ushawishi mkubwa kama Chadema na ACT-Wazalendo katika nafasi ya urais, jambo linaloweza kupunguza hamasa kwa wapigakura.

“Vyama hivi vina mashabiki wengi, hivyo kutoshiriki kwa wagombea urais wao kunaathiri mwamko wa wananchi,” anasema Dk Loisulie.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke, anasema vyama vinahimiza upigaji kura ili kupata uhalali wa kisiasa.

“Kauli za wanasiasa kama Humphrey Polepole na kampeni za ‘No Reforms, No Election’ zimeongeza msukumo huu mpya. Wanasiasa wanataka kuhakikisha matokeo yao yanatokana na ushiriki mpana wa wananchi,” anasema Dk Kyauke.

Anaongeza kuwa tofauti na miaka ya nyuma, mwaka huu hata chama tawala kinafanya kampeni katika maeneo ambako zamani kilihofia hamasa ya upinzani.

“Kwa mfano, mwaka 2015 CCM haikuwa rahisi kwenda Kaskazini kuhimiza watu wajitokeze kupiga kura, lakini mwaka huu wanafanya hivyo kwa sababu kinachotafutwa ni uhalali wa kisiasa,” anasema.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Bara) na mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Isihaka Mchinjita, anaema hali ya sasa inaakisi kupungua kwa imani ya wananchi baada ya matukio ya chaguzi zilizopita.

“Mazingira ya uchaguzi yamewakatisha tamaa wananchi wengi. Kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2019, ule wa 2020 na wa mwaka jana, matokeo yake yamepunguza imani ya watu,” anasema.

Hata hivyo, Mchinjita anasema ni wajibu wa vyama vya siasa kuhimiza watu wajitokeze kupiga kura.

“Pale watu wasipopiga kura, demokrasia inakufa. Katiba inasema mamlaka yatatokana na wananchi, hivyo wajitokeze kwa wingi kusimamia maamuzi yao,” anasema.

Mgombea urais wa NLD, Doyo Hassan Doyo, anasema kushuka kwa hamasa ya wapigakura kumewalazimu wanasiasa kutumia nguvu kubwa kuhamasisha wananchi kushiriki.

“Ukiona mwaka 2005 CCM ilipata asilimia 80.28, mwaka 2010 ilipata asilimia 61.17 na mwaka 2015 ilipata asilimia 58.46, yote haya yanaonesha idadi ya wapigakura na kura za ushindi zimekuwa zikishuka,” anasema Doyo.

Anaongeza kuwa mwaka huu wananchi hawana sababu ya kukata tamaa kwa kuwa kuna Tume Huru ya Uchaguzi.

“Waende wakapige kura waone uadilifu wa chombo hicho. Hamasa ni kubwa, hasa Dar es Salaam ambako tumekuwa na mikutano 19 yenye mwitikio mkubwa,” anasema Doyo.

Mkazi wa Ngerengere, Morogoro, Nurudini Mwadau, ameliambia Mwananchi kuwa idadi ndogo ya wapigakura inaweza kuathiri uhalali wa matokeo ya uchaguzi mkuu ujao.

“Hamasa imepungua kwa sababu wapinzani wakubwa hawapo kwenye kinyang’anyiro kama zamani. Kukosekana kwa ushindani kumesababisha kampeni nyingi kulenga zaidi kuhimiza watu wapige kura,” anasema.

Kwa upande wake, mkazi wa Kibaha mkoani Pwani, Asha Mwinuka, anasema wito wa kupiga kura unampa matumaini kuwa viongozi wameanza kuona umuhimu wa wananchi kushiriki moja kwa moja katika uamuzi.

“Zamani kila mtu alitaka tu uchague chama chake, sasa tunahamasishwa kupiga kura bila shinikizo. Hii inatufanya tujisikie huru kuchagua tunachotaka,” anasema Asha.

Mwananchi mwingine wa Dodoma, Rehema Ally, anasema anaona mwelekeo huo mpya wa wanasiasa ni hatua ya kuamsha ari ya wananchi waliokuwa wamekata tamaa na siasa.

“Kura ni silaha yetu. Wanasiasa wanaposema twende tukapige kura, wanatukumbusha wajibu wetu kama wananchi, si lazima niwe na chama chake ili niwe mzalendo,” anasema Rehema.