………………….
Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Tanzania imeendelea na Maandalizi kuelekea Mkutano
wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya
Tabianchi (COP30) utakaofanyika jijini Belem, Brazil Novemba 10 hadi 21, 2025.
Akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa wa Kimkakati
uliofanyika Dar es Salaam Oktoba 7,2025 Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya
Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amesema mikutano ya awali itasaidia kuweka
taswira ya nchi kuelekea COP 30.
“Tuna mambo yetu 14 ambayo tunakwenda kuyasema
kuwa msimamo wa Tanzania kuhusiana na masuala mbalimbali na katika kuendelea na
huu mkutano huu tunaangalia na tumeweza kuchambua nafasi ya nchi na tumepata
hoja za wadau ili kuiboresha,” alisema Msofe.
Ameelaza kuwa wamekumbusha kuna masuala ya Nishati,
Maji na uharibifu wa Mazingira ambapo hayo yote ni mambo ambayo watakwenda
kuyazungumza na lengo ni kwenda kuitangaza Tanzania.
“Dunia imejiwekea utaratibu wa masuala ya
Mabadiliko ya Tabianchi na mwaka huu Tanzania kama mdau wa masuala ya Mazingira
duniani itashiriki kupitia serikali, taasisi za umma mashirika yasiyo ya
kiserikalii na wadau wote wanaohusIka na masuala ya Mazingira,” aliongeza Prof.
Msoffe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa
la Mazingira (UNEP) nchini Tanzania Bi. Clara Makenya ameipongeza Serikali ya
Tanzania kwa kukutana na kupata uelewa wa pamoja kuelekea COP 30 mkutano
unaojumuisha wadau mbalimbali wa Mazingira kutoka maeneo tofauti tofauti.
“Wito wangu kuna mijadala mbalimbali na kila
mdau ana jukumu muhimu la kujiandaa kama
ni upande wa uchumi wa Buluu, Nishati au eneo lingine ajue eneo lipi anaenda
nalo kwa ajili ya kujipanga kimkakati na wadau wa dunia nzima na pia kujua kitu
gani anaenda kutoa na kujua mdau yupi anaenda kusapoti agenda anayoiwasilisha
na kufahamu kuwa wanaeda kama nchi na
kuweza kupata matokeo ambayo yanatarajiwa,” alisema Bi. Makenya.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa
Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Noel Kaganda amesema kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau wote wa serikali, wadau
kutoka sekta binafsi, Mashirika yasiyo
ya kiserikali juu ya maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.
“Janga hili la Mabadiliko ya Tabianchi linagusa
nchi zote, jamii zote, watu wa hali mbalimbali wenye kipato na wasio na kipato,
hivvyo ni jukumu letu kuchukua hatua za pamoja kukabiliana na mabadiliko ya
atabianchi, kujenga ustahimilivu na uendelevu,”
Amesema hilo linaenda na dira ya maendeleo ya nchi
ambayo hadi kufukia 2050 inataka kujenga jamii ambayo ni stahimilivi yenye
uchumi imara na inayomshirikisha kila mmoja katika jitihada za maendeleo.