TEF waitaka polisi kumtafuta Polepole, kuweka wazi kilichotokea

Dar es Salaam. Wakati watu wakiendelea kujiuliza wapi alipo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) nalo limejitokeza na kulitaka Jeshi la Polisi kuchunguza na kuweka wazi kilichotokea.

Pia, jukwaa hilo limehoji tabia hizi za kutekana zimetoka wapi wakati ambao Tanzania ni nchi ya amani.

Polepole anadaiwa kutekwa Oktoba 6, 2025 na watu wasiojulikana wakati ambao jeshi la Polisi likisema linaendelea kufanyia kazi madai hayo.

Kufuatia hilo, taarifa kwa vyombo vya Habari iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 8, 2025 na TEF imesema tukio hili linawakumbusha Watanzania matukio yaliyotangulia ya utekaji ya vijana Mdude Nyagali, Deusdedit Soka na wenzao.

“Jamii haijasahau pia mauaji ya kikatili ya Mzee Ali Kibao katika kipindi kifupi kilichopita,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deudatus Balile.

Wakati ndugu wa Polepole wakisema ametekwa akiwa Ununio, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, David Misime amesema wamepokea taarifa hizo na wanafanya uchunguzi.

Kilichosemwa na Misime kilikuwa tofauti na alichokisema Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ambaye alikaririwa na vyombo vya habari akihoji Polepole alikuja lini Tanzania, wakati muda wote amekuwa akijitaja kuwa yuko nje ya nchi.

Taarifa hiyo imesema Jukwaa la Wahariri Tanzania linaamini kuwa maisha na uhai wa Watanzania ni kipaumbele namba moja kwa amani ya Taifa.

Taarifa hiyo inasema amani ni tunda la haki huku TEF ikihoji tabia hizo zimetoka wapi. “Tunajiuliza tabia hizi zimetoka wapi? Nani anafanya utekaji huu? Watekaji wamepata wapi mafunzo haya? Wanaotekwa kwa nini wanatekwa? Kama ni siasa imekuwaje tukafika hapa? Je, tatizo ni tulipoangukia au kuna tulipojikwaa? Tunatokaje hapa,” imehoji taarifa hiyo kwa umma.

TEF imesema hata baada ya maswali hayo, Tanzania ni nchi ya amani, umoja, upendo na mshikamano, sifa wasiyotamani kuona inapotea.

“Wakati tunatafuta chanzo cha kadhia hii na majibu ya maswali haya, tunalisihi Jeshi la Polisi kuchunguza kwa haraka na kwa umakini taarifa hizi, kisha Taifa letu litangaziwe kwa uwazi nini kimetokea na nani mhusika na afikishwe mbele ya vyombo vya sheria haraka.

Hiyo ni kwa sababu TEF inaamini Tanzania ni nchi ya amani huku wakiweka bayana kuwa kama ni siasa, basi wafuasi wa vyama vya siasa na viongozi wao wanapaswa kupewa mafunzo ya kushiriki siasa zenye lengo la kuleta maisha bora kwa Watanzania, kwa kushindanisha hoja na si kuviziana kuangushana au kutekana.

“Kwa kauli moja tunasema, utekaji haukubaliki Tanzania,” imesema taarifa.

Kauli ya TEF inakuja ikiwa ni siku moja tangu taarifa kwa umma iliyotolewa na Jeshi la Polisi kupitia  Msemaji wa jeshi hilo, Misime kusisitiza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema linamsubiri Polepole ajitokeze na kuripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), kama lilivyoelekeza Septemba 15, 2025, wakati lilipotangaza kufungua jalada la uchunguzi kuhusu tuhuma zilizotolewa na mwanasiasa huyo.

Polepole alijiuzulu nafasi ya ubalozi Julai 13, 2025, akieleza kuwa hawezi kuendelea kushiriki katika uongozi usiozingatia utii wa katiba, haki, maadili, utu na uwajibikaji.

Usiku wa kuamkia Oktoba 6, 2025, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinadai kuwa Polepole ametekwa baada ya nyumba yake kuvunjwa na watu wasiojulikana.

Picha mjongeo zilizochapishwa mtandaoni zinaonesha milango na geti la nyumba hiyo vikiwa vimevunjwa, huku damu zikionekana kutapakaa ndani na nje ya nyumba hiyo inayodaiwa kukaliwa na Polepole.

Godfrey Polepole, aliyejitambulisha kama mdogo wa mwanasiasa huyo, akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC leo, Jumatatu Oktoba 6, 2025, amedai kuwa wamekuta nyumba ikiwa imevunjwa na damu zikiwa zimetapakaa ndani.

“Tulipofika, tumekuta nyaya za umeme zimekatwa, mlango wa geti kubwa umevunjwa na ndani kuna damu nyingi. Tulienda kutoa taarifa kituo cha Polisi, hali ni mbaya,” alidai mdogo wake huyo.