Na Pamela Mollel, Arusha
Zaidi ya wamama wadogo 180 kutoka jamii ya kifugaji katika kata ya Lemanyata, mkoani Arusha, wamenufaika na mradi wa ujasiriamali uliolenga kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii, pamoja na kuwasaidia kujitambua, kutoa maoni, na kusikilizwa ndani ya jamii zao.
Wamama hao ni wale wenye umri chini ya miaka 18, walio na watoto wasiozidi miaka mitatu au wakiwa wajawazito.
Akizungumza wakati wa matembezi maalum ya kuhitimisha mradi huo, yaliyokuwa na kauli mbiu “Nimejifunza, Nimeweza, Sasa Mniamini,” Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Builders of Future Africa (BFA), Elisante Ephrahim, alisema kuwa mradi huo wa mwaka mmoja ulianza Oktoba mwaka jana na sasa unakamilika kwa mafanikio makubwa.
Kabla ya kutekeleza mradi huo, alisema walifanya utafiti katika jamii za kifugaji na kubaini kuwa wengi wa mabinti wameolewa wakiwa wadogo au kupata mimba za utotoni kutokana na mila zao. Kupitia mradi huo, walipata fursa ya kujifunza na kujiendeleza kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
“Kila mmoja alieleza ndoto yake, nasi tukaanza mradi kulingana na mahitaji yao. Leo wanajitegemea na kujitafutia riziki kwa maarifa waliyopata,” alisema Ephrahim.
Ameeleza kuwa utafiti huo ulifanyika mwaka 2022, kipindi cha mlipuko wa COVID-19, katika kata tatu — Mwandeti, Lengijave na Lemanyata — ambapo walikutana na wamama wadogo 382 na kubaini changamoto zao. Mradi ulianza Lemanyata kwa lengo la kupunguza ongezeko la mimba za utotoni na kuwawezesha wasichana wadogo kujikwamua kiuchumi.
Ephrahim aliongeza kuwa baada ya mradi kukamilika, washiriki watawezeshwa mitaji na vifaa vya kuanzishia biashara kulingana na mafunzo waliyopata, kabla ya mradi kuhamia kata nyingine.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa BFA, Daniel Msigwa, alisema shirika hilo linafanya kazi kwa ushirikiano na Little Prospect Foundation pamoja na Her Journey to School, huku CRVPF ikiwa mfadhili mkuu wa mradi.
“Tunafanya kazi katika vijiji vitatu vya kata ya Lemanyata. Lengo ni kutatua changamoto za mabinti wadogo waliopata ujauzito wakiwa na ndoto ambazo hazikutimia. Tunawapa mafunzo ya ujasiriamali kama ushonaji, upishi wa keki, utengenezaji wa sabuni, shanga, lishe bora, na elimu ya utunzaji wa fedha kupitia vikundi,” alisema Msigwa.
Aidha, wamama hao wadogo wamewezeshwa kuanzisha vituo vinne vya malezi kwa watoto wao wapatao 192, katika vijiji vitatu hivyo. Vituo hivyo vinatoa elimu ya awali na huduma ya lishe, ili kuwawezesha wamama kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Little Prospects Foundation, Fauster Muttani, alisema kuwa mradi huo umeleta matumaini mapya kwa wamama wadogo waliokuwa wamekata tamaa.
“Ndoto za wengi wao zilizimika mapema kutokana na ujauzito wa utotoni. Tuliona ni muhimu kuwasaidia kuandika historia mpya katika maisha yao na jamii zao,” alisema Muttani.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Anna Thomas, alisema kuwa mradi huo umewapa uwezo wa kujiamini na kushiriki katika maamuzi ya kifamilia.
“Tulikuwa tukikaa nyumbani bila kazi. Sasa tunajitegemea, tunashona, tunatengeneza sabuni, na tunaweza kutunza familia zetu. Huu mradi umetubadilishia maisha,” alisema kwa furaha.
Mradi wa wamama wadogo wa Lemanyata umeonekana kuwa mfano wa mafanikio ya juhudi za kuleta usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake wadogo katika jamii za kifugaji, ukionesha njia ya matumaini na mabadiliko endelevu.