Wananchi wahamasishwa kujitokeza kupima saratani

DAKTARI Bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Kezia Tessua, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao, hususan magonjwa yasiyo ambukiza kuepuka madhara.

Kezia, alitoa wito huo, Bunju, Dar es Salaam, juzi katika Programu ya Viongozi Wanawake, inayosimamiwa na Taasisi ya Uongozi.

Alisema kwamba, baadhi ya magonjwa hayo ni saratani, shinikizo la damu na kupanda kwa sukari katika damu.

“Tuko hapa katika programu hii ya wanawake viongozi kupima na kung’amua magonjwa katika dailili za mwanzoni, tutaangalia kupanda shinikizo la damu, sukari katika damu, saratani za shingo ya kizazi, matiti. Magonjwa hayo, yanajulikana siyo ya kuambikiza”, alisema.

Kezia, alisema magonjwa hayo kwa sasa, yanasababisha vifo vingi, kwani zaidi ya robo tatu ya vifo vyote vinavyotokea duniani, vinatokana na magonjwa hayo, hivyo wananchi wanapopata nafasi, wapime afya kuepuka madhara.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi waMafunzo kwa viongozi kutoka Taasisi ya Uongozi, Emmanuel Tessua, alisema wameshirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika mafunzo hayo, kuwapa fursa wanawake viongozi kupima magonjwa yasiyoambukiza.

“Tumekuwa tukishirikiana nao wenzetu wa taasisi ya saratani, tunapokuwa na mafunzo, viongozi wanapata nafasi ya kupima afya zao kama magonjwa yasiyoambukiza, kwa mfano saratani ya shingo ya kizazi na matiti”, alisema.

Tessua, alisema pamoja na kuwapa mbinu za uongozi, programu hiyo, imewasaidia kuimarisha katika suala la afya.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo, Susan Mark, alisema amefarijika na huduma hiyo ya kupima afya kutoka taasisi ya Saratani ya Ocean Road, hususan saratani ya kizazi na matiti, ingawa  mwanzoni alikuwa anaogopa.

“Nashukuru nimepima baada ya kuona huduma nzuri,nimepata ushauri mzuri, nimefahamu kwa nini nipime kujua hali yangu, haswa saratani, ugonjwa huo ukigundulika mapema, unatibika, hata wenzetu walitoa ushuhuda kuwa, walipata saratrani, baada ya matibabu, wamepona”, alisema.

Susan, alisema jamii wapate muda wa kuangalia afya zao, hasa wanawake, wanaweza kujipima wenyewe nyumbani, wakibaini dalili za saratani waanze matibabu mapema.